Rais wa Seychelles Wavel Ramkalawan ni miongoni mwa viongozi wa Afrika wanaosherehekea Siku ya Madaraka na Kenya mwaka huu.
Pia yumo aliyekuwa Rais wa Niger Mahamadou Issoufou ambaye alikaribishwa na Naibu Rais Rigathi Gachagua na mkewe Mchungaji Dorcus Gachagua.
Rais wa Comoros Azali Assoumani pia anahudhuria.
Takriban watu 10,000 wanahudhuria sherehe za 60 za Madaraka za Kenya katika Kaunti ya Embu.
Rais William Ruto aliwasili katika uwanja wa Moi, kaunti ya Embu mwendo wa saa tano asubuhi kuongoza taifa katika Maadhimisho ya Siku ya Madaraka.
Hii ni mara ya tatu kwa Ruto kuongoza nchi kuadhimisha Sikukuu ya Kitaifa tangu aingie madarakani Septemba 13, 2022.
Rais aliandamana na Mkewe Rais Rachael Ruto.
Rais alikagua gwaride la heshima lililowekwa na Wanajeshi wa Kenya kabla ya kuongoza nchi katika sherehe za Madaraka Dei.
Ruto anatarajiwa kuongoza sherehe hiyo ambayo kilele chake kitakuwa hotuba ya rais inayotarajiwa kuangazia safari ya nchi baada ya uhuru.
Hotuba yake pia itaangazia baadhi ya mafanikio yake na pia kuonyesha maono yake kwa nchi.