Viongozi wa Afrika wametakiwa kuungana na kuwa na kauli moja katika juhudi za kukabiliana na maendeleo ya uchumi, mabadiliko ya hali ya hewa na umaskini unaolikumba bara la Afrika.
Akizungumza katika siku ya pili ya mkutano wa mabadiliko ya hali ya hewa siku ya Jumanne katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesisitiza umuhimu wa uwepo wa kauli moja katika kufanikisha jitihada hizo.
Mkutano huo ambao umehudhuriwa na marais wasiopungua kumi na watano kutoka nchi mbalimbali za Afrika ulijadili mchango wa nchi zao katika ufanikishaji wa nguvu za pamoja ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Pia wakuu hao wa nchi wamejadili ufadhili unaohitajika ili kuimarisha nguvu za kijamii katika kukabiliana na athari za mabadiliko hayo, pamoja na mishtuko mingine inayohusiana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Amesema ili kupata suluhu zinazohusu mwiitikio wa juhudi za kukabiliana na maendeleo ya uchumi, mabadiliko ya hali ya hewa na umaskini barani Afrika, viongozi hawafai kujitenga.
Mwenyeji wa mkutano huo, Rais William Ruto, kwa mara nyingine ameulalamikia mfumo wa kifedha wa ulimwengu usio na usawa, na kutoa wito wa kufanyika mabadiliko muhimu.
Ruto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa, ameuelezea mkutano huu kuwa ni wa kipekee kwa wakuu wa nchi za Afrika, ambao unatoa fursa katika ubadilishanaji mawazo kuwa vitendo, na kubadilisha mipango kuwa matokeo halisi na chanya na kuunda makubaliano thabiti na kubuni mikakati madhubuti.
Amesema mkutano huo unatoa fursa ya kupata ahadi na kuunda ushirikiano wa mageuzi ambao utaendesha hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa katika mwelekeo na kwa kiwango kinachohitajika ili kuliwezesha bara la Afrika kuondoka kwenye ukingo wa janga la mabadiliko hayo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anawaomba viongozi wa Afrika kuchukua hatua na kukabiliana na hali mbaya ya hewa na kukariri kuwa ukosefu wa haki umejikita ndani ya mzozo wa mabadiliko ya tabianchi na mwali wake unachoma matumaini na uwezekano barani Afrika.
Rais wa Rwanda, Paul Kagame, ameeleza kuwa lazima viongozi waondokee mchezo wa lawama kwa sababu sio jibu, bali viongozi hao wanastahili kuelekea katika mtazamo wa kisayansi unaonyesha kuwa Afrika ni mdau muhimu katika kutafuta suluhu za mabadiliko ya hali ya hewa duniani.
Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo amesema kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi hazikomei barani Afrika na viongozi ni vyema wahakikishe uwepo wa mustakabali endelevu kwa vizazi vijavyo.
Rais wa Sierra Leone Julius Maada Bio anasema kuwa ushirikiano utazisaidia nchi za Afrika kukabili mabadiliko haya na kufikia uungwaji mkono wa kimataifa kuekelea ukamilishaji wa ukuaji wa kijani kwa nchi na siyo kukaidi.
Mjumbe maalum wa hali ya hewa wa Marekani John Kerry ametangaza kitita cha dola milioni 30 kutoka serikali ya Marekani ili kuharakisha juhudi za utoshelevu wa chakula kwa mazao yanayostahimili mabadiliko ya tabianchi kote barani Afrika.
Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Akinwumi Adesina amewataka viongozi wa Afrika kulinda maisha ya watu kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa kwa sababu yanapunguza uwezo na nguvu za bara la Afrika.
Frederick Kihara kutoka shirika la kimataifa la Nature Conservancy, anaeleza kuwa ufadhili wa fedha wa ulimwengu haufiki barani Afrika na hili hutatiza kwa kiasi kikubwa nguvu za kukabili changamoto za hali ya hewa.
Wajumbe wanaojumuisha wakuu wa nchi, watunga sera, viongozi wa serikali, watoa maamuzi, wataalam wa mabadiliko ya tabianchi, mashirika ya kimataifa na mashirika ya kiraia, na sekta binafsi wanatakiwa kutafuta ufumbuzi wa mabadiliko ya tabianchi barani Afrika kwa kuongeza juhudi zilizopo na kuepuka mtego wa mazungumzo yasiyokwisha na yasiYokuwa na vitendo halisi.