Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Viongozi EAC kumuunga mkono Odinga uenyekiti AUC

Mgogoro Wa Haiti Sio Kipaumbele Cha Kenya   Odinga Viongozi EAC kumuunga mkono Odinga uenyekiti AUC

Thu, 7 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), watamuunga mkono mgombea mmoja wa uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

Hayo yametangazwa jijini Nairobi juzi na Rais wa Kenya, William Ruto alipohutubia Bunge la Afrika Mashariki (Eala).

Wagombea wawili kutoka EAC ni Raila Odinga wa Kenya na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia, Fawzia Yusuf Adam.

Hata hivyo, wakati wa hotuba yake, Ruto ameliambia Bunge la EAC kuwa marais wa Afrika Mashariki wamekubali kumuunga mkono mgombea mmoja wa kiti cha uenyekiti.

“Tumekaa chini kwa moyo wa EAC, tumeshauriana kama wakuu wa nchi na tumekubaliana kuweka mgombea mmoja", alinukuliwa Ruto na vyombo vya habari vya Kenya.

Kwa mujibu wa Ruto, uamuzi huo umefikiwa baada ya mashauriano ya kina… “Tutadhamini mgombea mmoja kama Waafrika mashariki kwa sababu hiyo ndiyo nguvu ya jumuiya yetu," amesema.

Kugombea kwa Raila kuwa Mwenyekiti wa AUC kumezua mjadala katika siasa za Kenya, ikizingatiwa kuwa alikuwa mpinzani mkubwa wa Rais Ruto.

Tangu habari za kugombea kwake kutangazwa hadharani, kiongozi huyo wa upinzani amepunguza mashambulizi yake ya maneno dhidi ya Serikali ya Ruto.

Kambi ya upinzani nayo haijasalimika kwa sababu imejikuta ikigawanyika, huku wengine wakitabiri mwisho wa changamoto kali za moja kwa moja kwa Serikali iliyoko madarakani. Vyombo vya habari vya Kenya hivi karibuni vimekuwa vikiripoti uwezekano wa kuvunjika kwa muungano wa Azimio la Umoja unaoongozwa na Raila.

Muungano wa Azimio la Umoja unahusisha Chama cha ODM chenye ngome kubwa magharibi mwa Kenya na Jubilee inayohusishwa na rais wa zamani, Uhuru Kenyatta.

Wachambuzi wengine wanaamini kuchaguliwa kwa Raila kama mwenyekiti wa AUC, kutashuhudia kuondoka kwake kutoka kwa upinzani mkali katika siasa za mitaa za Kenya na hivyo kuleta ahueni kwa Kenya Kwanza.

Hata hivyo, Raila amekanusha hilo mara kwa mara, akisisitiza bado angetekeleza wajibu wake katika siasa za upinzani, licha ya kufurahia kuungwa mkono na Ruto katika kuwania nafasi hiyo ndani ya AUC.

Aidha, wakati wa hotuba yake, Ruto pia alisema usalama uliopo katika ukanda wa Afrika Mashariki umechangia ukuaji mkubwa wa EAC, na kuifanya kuwa kitovu chenye ushindani wa kibiashara kote ulimwenguni.

Kulingana na kiongozi huyo wa Kenya, Afrika Mashariki inaibuka kuwa kinara wa umoja, utulivu, usalama na maendeleo na kiungo muhimu katika ushirikiano na uanamajumui.

Pia ametangaza kuwa Kenya itakuwa mwenyeji wa mkutano wa mwaka huu wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Benki ya Dunia (IDA) Aprili 29, 2024. Mkutano huo utalenga kusaidia mageuzi ya kiuchumi barani Afrika na kote Kusini mwa ulimwengu, alidokeza.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live