Vikosi vya usalama vya Uganda vimesema vimenasa vilipuzi vilivyokusudiwa kutumiwa wakati wa maandamano ya kuipinga serikali yaliyopangwa kufanyika katika mji mkuu Kampala.
Kundi la wanaharakati, Wanaharakati wa Uhuru wa Uganda, limeitisha maandamano nchi nzima siku ya Jumatatu kupinga ufisadi na hali ngumu ya kiuchumi nchini humo.
Msemaji wa ulinzi, Brig Felix Kulayigye, kwenye tweet alisema vilipuzi vilipatikana Nabweru kwenye barabara ya kuelekea Kazo katikati mwa wilaya ya Wakiso.
"Hizi zingetumiwa leo jijini na wale wanaopanga kuipaka rangi nyekundu," Brig Kulayigye alisema.
Polisi walionya wanaharakati hao dhidi ya kuandaa maandamano hayo, wakiyataja kuwa ni kinyume cha sheria.
Wanaharakati hao, hata hivyo, wameapa kuendelea na maandamano, wakimuelezea Brig Kulayigye kama "mwongo".