Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vijana 34 Afrika Kusini wafariki dunia jandoni

Vijanapic Data Vijana 34 Afrika Kusini wafariki dunia jandoni

Mon, 27 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Badala ya kusherehekea ujio wa watoto wao wa kiume, mwezi huu familia 34 katika Jimbo la Eastern Cape Afrika Kusini zinaomboleza vifo vyao.

Takriban wavulana 34 wamefariki dunia mwezi huu wakati wa jando. Tume ya kutetea haki za kitamaduni Afrika Kusini inataka kuzuiliwa kwa shule zinazotoa mila hiyo hatari ili kuzuia vifo zaidi.

Unyago huo ni utamaduni wa kawaida, hasa miongoni mwa Waxhosa, lakini pia ni hatari na unaweza kusababisha kifo.

Kila mwaka, wavulana huacha familia zao kwenda kukaa kwa wiki moja au zaidi na kiongozi wa kimila nyikani na wao pia hutahiriwa.

Maofisa wa Afrika Kusini wanahangaika kuelewa ni nini kilitokea hadi wavulana hao wakafariki dunia.

David Luka Mosoma ni mwenyekiti wa Tume ya Kukuza na Kulinda Haki za Jumuiya za Kiutamaduni, Dini na Lugha.

Advertisement “Hakuna Taifa linalojivunia kufanya mauaji ya watoto wake na hakuna utamaduni unaoweza kulaumiwa kwa hili kwa sababu vifo hivi ni matokeo ya uzembe wa kibinadamu, ikiwa ni pamoja na vitendo vya uhalifu vinavyoendelea hivi sasa na biashara ya mila hiyo,” alisema Mosoma.

Polisi wa Afrika Kusini wanachunguza vifo hivyo, ambavyo Serikali ilisema inaonekana vilitokana na tohara, uzembe na unyanyasaji.

Mapema mwezi huu, Serikali ilisema mvulana mmoja alikufa maji baada ya kiongozi wake wa kimila kumlazimisha kuogelea.

Mkuu wa Jimbo la Eastern Cape, Oscar Mabuyane aliwaambia waandishi wa habari kuwa, jamii lazima zichukue jukumu zaidi ili kuhakikisha usalama wakati wa jando.

“Matatizo mbalimbali yangeweza kuepukika kama wanaume katika jamii wangeshiriki kwa usalama jukumu lao katika mchakato huo,” alisema Mabuyane.

“Unawaelezaje kina mama wa wavulana hawa kwamba walikufa wakiwa chini ya uangalizi wetu kwa sababu ya majeraha, upungufu wa maji mwilini na kushambuliwa?” alisema Mabuyane.

Tume ya Haki za Kitamaduni inasema takriban vijana 700 wamekufa katika mwongo mmoja uliopita wakati wa mila ya jando, huku wengine wengi wakikumbana na matatizo yanayosababishwa na tohara.

Licha ya hasira ya umma iliyosababishwa na vifo hivyo, kuharamisha mila ya mababu nchini Afrika Kusini si chaguo lao.

Mwanasaikolojia wa Tiba katika Kituo cha Afya cha Familia ya Ubuntu, Anele Siswana, anajifunza taratibu za unyago huo na matokeo yake.

Alisema mila hiyo ni muhimu sana kwa jamii.

“Kuna mahali na umuhimu unaohusu mchakato huu. Unahusiana sana na kuwasaidia wavulana wachanga kuwa wanaume bora... inawafundisha ni nini maana ya mtu anayewajibika, anayeihudumia familia, anayeilinda familia, na uhuru wa mtu na utu,” alisema Siswana.

Siswana alisema shughuli ya mila hiyo imechangia kuongezeka kwa shule haramu zinazowania kupata faida.

Shule haramu za unyago zimelaumiwa kwa wingi wa vifo vya hivi majuzi.

Afrika Kusini ina sheria za kuhakikisha usalama wa wenye shule hizo za kimila, lakini mwenyekiti wa tume ya haki, Mosoma alisema fedha na rasilimali zinazohitajika kutekeleza kanuni zinakosekana.

“Mahakama maalumu inapaswa kuanzisha mashtaka ya haraka na kushughulikia uhalifu unaohusiana na unyanyasaji,” alisema Mosoma.

“Hakuna mtu anayepaswa kuachwa kwa kufanya ukiukaji mkubwa au uzembe mkubwa.”

Wakati huo huo, Tume ya Afrika Kusini ya Kukuza na Kulinda Haki za Jumuiya za Kitamaduni, Dini na Lugha inataka shule zisizo halali zifungwe mara moja na zilizosajiliwa zifuatiliwe kwa karibu zaidi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live