Maafisa wawili waandamizi wa jeshi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wametiwa mbaroni baada ya kudaiwa kutoa amri ya kutumika kwa nguvu kufanya mauaji dhidi ya maandamano yaliyopigwa marufuku.
Vikosi vya usalama viliingilia kati wakati maandamano dhidi ya walinda amani wa kimataifa yakiendelea Jumatano iliyopita na watu 43 waliuawa na wengine 56 kujeruhiwa.
Waandamanaji hao walikuwa wa madhehebu mbalimbali ya kidini na walikuwa wakitaka vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Afrika Mashariki viondolewe katika maeneo yao.
Maafisa waliokamatwa ni Mike Mikombe, mkuu wa walinzi huko Goma, na Donat Bawili, kiongozi wa jeshi mjini humo, kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani Peter Kazadi. Haijabainika ni mashtaka gani watakabiliwa nayo.
Waziri huyo aliahidi kuwa uchunguzi kuhusu mauaji hayo, ambayo yalizua ghadhabu ya kitaifa na kimataifa, utakuwa wa wazi.