Watoto wawili wameokolewa wakielea karibu na ufukwe wa ziwa Kivu siku chache baada ya mafuriko kuua zaidi ya watu 400 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
"Ni muujiza, sote tulishangaa," kiongozi wa jumuiya ya eneo hilo Delphin Birimbi aliiambia BBC.
Wazazi wao wamefariki lakini jamii inawasiliana na watu wanaoweza kuwalea, ameongeza Birimbi.
Haijabainika jinsi watoto hao wachanga walivyonusurika kwa siku tatu katika ziwa hilo, lakini mashuhuda wanasema walionekana wakiwa wanaelea.
Watoto hao waliokolewa Jumatatu, mmoja huko Bushushu na mwingine Nyamukubi, vijiji viwili vilivyoathiriwa zaidi na mafuriko yaliyotokea wiki jana, amesema Birimbi.
Maiti zaidi zilipatikana kwenye tope siku ya Jumatano, na kufanya idadi ya waliofariki kufikia 411, ambapo kati ya marehemu hao, 317 wamezikwa.
Hata hivyo, kuwatambua marehemu wote ni changamoto, viongozi wa eneo hilo wanasema, kwa kuwa baadhi yao hawakuwa wakazi wa vijiji hivyo, bali wafanyabiashara waliokuwa wakitembelea kutoka miji ya jirani kutokana na mvua kunyesha siku ya soko.
Mwakilishi kutoka shirika la matibabu la Médecins Sans Frontières (MSF) awali alielezea ukubwa wa maafa katika mahojiano na kipindi cha Newsday cha BBC, akisema kwamba vijiji vinakabiliwa na mahitaji mengi ya kibinadamu.