Utulivu ulirejea katika mji mkuu wa Burkina Faso siku ya Jumatatu baada ya kiongozi wa kijeshi wa nchi hiyo kukimbilia nchi jirani ya Togo kufuatia mapinduzi ya pili katika muda wa chini ya miezi tisa.
Mitaa ya Ouagadougou ilikuwa tulivu baada ya mzozo wa siku mbili kati ya mkuu wa utawala wa kijeshi Luteni-Kanali Paul-Henri Sandaogo Damiba na mpinzani mpya aliyeibuka kuwania mamlaka, Kapteni Ibrahim Traore mwenye umri wa miaka 34.
Baada ya wikendi ya mtafaruku ambayo pia ilishuhudia maandamano yenye vurugu katika ubalozi wa Ufaransa na kituo cha utamaduni, Damiba alikubali Jumapili kujiuzulu.
Wanadiplomasia walisema Damiba alienda katika mji mkuu wa Togo Lome, na hilo lilithibitishwa siku ya Jumatatu na serikali ya Togo, ambayo ilisema imemkubali ili kuunga mkono amani katika kanda hiyo ndogo.
Katika video iliyotolewa Jumatatu, Damiba aliwatakia kila la kheri wale waliompindua, akiwataka kuungana badala ya kugawanyika.