Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Utafiti wabaini asilimia kubwa vijana Afrika wanavyotumia fedha kucheza kamari

91999 Betting+pic Utafiti wabaini asilimia kubwa vijana Afrika wanavyotumia fedha kucheza kamari

Thu, 16 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Utafiti uliofanywa na taasisi ya utafiti ya GeoPoll ukihusisha nchi sita za Afrika katika matumizi ya simu na fedha umebaini asilimia 28 ya vijana wanatumia fedha mtandaoni katika matumizi yanayofanana.

Utafiti huo ulihusisha nchi za Kenya, Tanzania, Uganda, Ghana, Nigeria na Ivory Coast umehusisha vijana 400 wenye umri kati ya miaka 18 hadi 35 kwa kila nchi.

Data za utafiti huo zilijikita zaidi kwenye kundi kubwa la watu wenye simu na huduma ya mtandao wa internet ambao waliwakilisha jamii nzima ya watu wanaotumia huduma za kibenki na huduma za malipo kwa njia ya simu.

Utafiti huo ulibaini asilimia 28 ya vijana wanatumia fedha mtandaoni kufanya malipo katika shughuli za kamari, matumizi ya mtandao majumbani, kununua muda wa hewani kwenye simu na kulipia chaneli za televisheni kwa kutumia simu.

Kwa mujibu wa Geopoll matokeo ya utafiti wao yalionyesha asilimia 63 ya watu waliohojiwa kuhusu matumizi ya fedha kwenye simu zao walisema wanatumia fedha kucheza kamari mtandaoni au huku asilimia 54 wanatumia fedha kwenye simu kulipia huduma za mtandao (Internet).

Geopoll wamebainisha asilimia 53 ya waliohojiwa walijibu wanatumia fedha zao kwenye simu kununua muda wa hewani kwenye simu zao huku asilimia 53 wanatumia zaidi kufanya malipo ya kwenye televisheni.

Ripoti hiyo ya Geopoll imeendana na ripoti nyingine zilizowahi kuonyesha kamari kwa njia ya mtandao na hata zile za nje ya mtandao ni tatizo kubwa barani Afrika huku kubeti kwa ajili ya mchezo wa soka kukichochewa na ushabiki wa timu za soka za Ulaya huku kubeti huko kukiathiri matumizi ya fedha kwenye simu.

 

Katika utafiti huo uliohusisha nchi mbalimbali Kenya imeonekana kuongoza kwa kuwa na vijana wengi ambao wanacheza kamari na kubeti na wamiliki wa akaunti milioni 12 za kubeti  wakipoteza takriban Dola za Marekani bilioni mbili kila mwaka.

Tovuti 12 zinazoongoza kwa michezo ya kubeti nchini Kenya zimekuwa zikivuna mapato ya zaidi ya Sh 250 bilioni ambayo ni zaidi ya bajeti ya taifa hilo.

Kuongezeka huko kwa matumizi ya fedha kwa njia ya simu kumesababisha watu wengi kuwa na uraibu, umaskini na matatizo ya kiakili ikiwamo kujiua.

Nchini Kenya asilimia 82 ya vijana wanatumia fedha kwenye simu kubeti au kamari, asilimia 71 wanatumia fedha kwenye simu kulipia huduma ya mtandao (Internet), asilimia 82 wanatumia kulipia chaneli za  televisheni  na asilimia 64 ndiyo hutumia fedha zao kwenye simu kununua muda wa hewani wa simu.

Rais Uhuru Kenyata wa Kenya aliwahi kusema ataunga mkono kufungwa kabisa kwa michezo ya kamari nchini humo licha ya wengi kuona kama itakuwa tishio kwa kodi japo jambo hilo limezua sintofahamu kwa mustakabali wa maisha ya watu.

Hali ilivyo Uganda, Tanzania

Nchini Uganda, asilimia 75 ya waliohojiwa walisema wanatumia fedha kwenye simu zao kucheza kamari na kubeti huku asilimia 72 wakisema wanatumia zaidi kulipia huduma ya mtandao (internet), asilimia 79 wakisema wanatumia zaidi kulipia chaneli za televisheni na asilimia 62 wakisema wanatumia zaidi pesa hizo kununua muda wa hewani wa simu.

Tanzania imeonekana kuwa nchi ya tatu barani Afrika kwa vijana kutumia fedha zaidi kwenye simu kucheza kamari au kubeti kwa mujibu wa utafiti wa Geopoll.

Nchini Tanzania asilimia 76 ya waliohojiwa walisema wanatumia fedha za kwenye simu kucheza kamari au kubeti, asilimia 72 walisema wanatumia kununua huduma ya mtandao (Internet), asilimia 74 walisema wanatumia zaidi kulipia chaneli za televisheni, na asilimia 64 ndio wanatumia pesa kwenye simu kununua muda wa hewani.

Nchini Ghana pia suala la kamari na kubeti limeonekana kushabihiana na Tanzania ambapo asilimai 76 ya waliohojiwa pia walisema wanatumia fedha kwenye simu zao kucheza kamari au kubeti, asilimia 51 wakisema wanatumia zaidi kununua huduma ya mtandao, asilimia 57 wanatumia kulipia chaneli za televisheni na asilimia 60 ndio hutumia kununua muda wa hewani.

Nchi ya Ivory Coast utafiti wa Geopoll ubaini asilimia 40 tu ya watumiaji wa simu waliohojiwa ndio wanatumia fedha zao kwenye simu kucheza kamari, huku asilimia 34 wakisema wanatumia kununua muda wa hewani, asilimia 25 walisema wanatumia kununua huduma ya mtandao (Internet) huku kukiwa hakuna aliyesema anatumia simu kulipia chaneli za televisheni

Nigeria ilionekana kushika mkia katika suala la uchezaji kamari au kubeti miongoni mwa nchi hizo sita zilizofanyiwa utafiti.

Watu waliohojiwa nchini Nigeria kuhusu wapi wanakotumia zaidi fedha zao za kwenye simu utafiti ulionyesha asilimia 27 wanatumia kucheza kamari au kubeti, asilimia 35 wanatumia kununua huduma ya mtandao (internet), asilimia 28 hulipia chaneli za televisheni na asilimia 32 ndio hutumia kununua muda wa hewani.

Chanzo: mwananchi.co.tz