Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ushelisheli: Mwanasiasa wa upinzani ashtakiwa kwa kesi ya uchawi

Ushelisheli: Mwanasiasa Wa Upinzani Ashtakiwa Kwa Kesi Ya Uchawi Ushelisheli: Mwanasiasa wa upinzani ashtakiwa kwa kesi ya uchawi

Tue, 3 Oct 2023 Chanzo: Bbc

Mahakama moja nchini Ushelisheli imemshtaki kiongozi wa chama kikuu cha upinzani na watu wengine saba kwa tuhuma za uchawi.

Patrick Herminie anapanga kugombea katika uchaguzi wa urais wa 2025 chini ya bendera ya United Seychelles Party (USP), chama kikuu cha upinzani nchini humo.

Hata hivyo, amekanusha mashtaka hayo.

Aliambia vyombo vya habari vya ndani kuwa kukamatwa kwake na kufunguliwa mashtaka ni juhudi za kisiasa za kuchafua taswira yake na ya chama chake.

Polisi wanasema kisa hicho kinahusiana na kupatikana kwa miili miwili iliyokuwa imetolewa kwenye makaburi katika kisiwa cha Mahe.

Kulingana na ripoti za vyombo vya habari nchini, Bw Herminie na washtakiwa wenzake wanakabiliwa na mashtaka kadhaa, ikiwa ni pamoja na kupatikana na vitu vilivyokusudiwa kutumiwa katika uchawi na kula njama ya kufanya uchawi.

Polisi wanasema walimpata Bw Herminie akiwa na stakabadhi zinazoshukiwa kuibwa kutoka maeneo yaliyoharibiwa, yakiwemo makanisa ya Kikatoliki.

Pia wanadai kuwa jina la Bw Herminie lilionekana kwenye mawasiliano ya Whatsapp kati ya raia wa Ushelisheli na Mtanzania ambaye alikamatwa Septemba akiwa na vitu vinavyohusiana na uchawi.

Mahakama ilimwachilia Bw Herminie na washtakiwa wengine wa Ushelisheli kwa dhamana ya rupia 30,000 za Ushelisheli ($2,100; £1,745), lakini mshukiwa wa Tanzania atakaa rumande hadi kusikizwa kwa kesi hiyo mwezi Novemba.

Chanzo: Bbc