THAMANI ya usafirishaji wa bidhaa kwenda nje ya nchi imeongezeka kwa asilimia 6.4 katika kipindi cha miezi 10 hadi kufikia Oktoba, mwaka jana licha ya changamoto za virusi vya corona kwenye biashara ya kimataifa.
Ofisi ya Kitaifa ya Takwimu ya Kenya hivi karibuni ilisema katika kipindi hicho jumla ya mauzo ya nje yalifikia kiwango cha juu cha Sh bilioni 532.9 ikilinganishwa na Sh bilioni 499.9 kipindi kama hicho mwaka uliopita.
Usafirishaji wa ndani kutoka Kenya kwa Januari hadi Oktoba, mwaka jana ilikuwa Sh bilioni 464.9 kukiwa na ongezeko ikilinganishwa na usafirishaji wa Sh bilioni 437 uliosafirishwa nje ya nchi kipindi kama hicho mwaka 2019.
Aidha, thamani ya jumla ya kuagiza bidhaa kwa mwaka hadi kufikia Oktoba, mwaka jana ilikuwa Sh trilioni 1.341 ambayo ni pungufu ikilinganishwa na Sh trilioni 1.486 kipindi kama hicho mwaka uliopita.
Janga la covid-19 limepunguza pato la viwanda ulimwenguni kutokana na kuathiri mifumo ya biashara ya kimataifa na usafirishaji na kusababisha biashara ya Kenya na washirika wake wakuu kushuka hadi Sh trilioni 1.874 kutoka Sh trilioni 1.987 kipindi kama hicho mwaka 2019.
Pakistan ambayo inachukua asilimia 38 ya mauzo ya chai ya Kenya ilikuwa soko la pili la kuuza nje licha ya kushuka kwa idadi ya chai iliyouzwa tangu mwanzo wa janga hilo Machi, mwaka jana.
Masoko mengine makuu ya bidhaa za Kenya ni Uholanzi (hasa maua), Uingereza, Marekani, Tanzania, Misri, Rwanda, UAE, Ujerumani na Ufaransa.