Muungano wa upinzani wa National Salvation Front nchini Tunisia ulisema siku ya Alhamisi kwamba utafanya maandamano siku ya Jumapili licha ya kunyimwa kibali na mamlaka nchini humo, huku kukiwa na msako mkali dhidi ya wakosoaji wakuu wa rais wa nchi hiyo.
Upinzani wa Tunisia unatazama jinsi mamlaka itakavyoshughulikia maandamano hayo na mengine yaliyoitishwa Jumamosi na chama chenye nguvu cha wafanyakazi, UGTT, kutokana na kukamatwa mfululizo kwa wakosoaji mashuhuri wa Rais Kais Saied.
Gavana wa Tunis alisema katika taarifa yake kuwa anakataa kutoa kibali cha maandamano ya Jumapili kwa sababu viongozi wa kundi hilo wanatuhumiwa kula njama dhidi ya usalama wa taifa.
Viongozi wa muungano wa National Salvation Front ni miongoni mwa wapinzani kadhaa wa rais waliokamatwa mwezi mmoja uliopita kwa madai ambayo upinzani unasema yanachochewa kisiasa.