Kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe Nelson Chamisa amesisitiza kutoyatambua matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi Rais Emmerson Mnangagwa.
Nelson Chamisa badala yake amedai kwamba, yyeye ndiye mshindi katika uchaguzi ambao waangalizi wa kimataifa wameuelezea kuwa, haukukidhi viwango vya kidemokrasia.
Muungano wa upinzani wa wananchi kwa ajili ya mabadiliko umekataa matokeo ya uchaguzi huo na kudai yalikuwa matokeo ya "uongo."
Chamisa, wakili na mchungaji wa kanisa amewaambia waandishi wa habari katika mji mkuu Harare kuwa, muungano wa CCC ndio ulioshinda uchaguzi huo na anashangaa kwa nini Mnangagwa ametangazwa mshindi.
Rais mteule wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa ametupilia mbali ripoti za baadhi ya waangalizi wa kimataifa waliopinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.
Mnangagwa alikuwa akitoa hotuba yake ya kusherehekea ushindi hapo jana na kusema kwamba alishinda uchaguzi kwa haki na hatakengeushwa na maoni mengine. Rais Emerson Mnangagwa ameshinda kiti cha urais kwa mujibu wa matokeo ya Tume ya Uchaguzi ya Zimbabwe
Ameongeza kuwa, "Ninafahamu kuwa baadhi ya wajumbe wa waangalizi walivuka wajibu wao na kuanza kuhoji sheria iliyopitishwa na bunge letu. Kila nchi huru inapitisha sheria yake kupitia bunge lao na Zimbabwe pia ilifanya hivyo." Aidha amesema hakusimamia uchaguzi bali alishiriki kama mshindani na kuongeza kuwa:
Mnangagwa ameshinda uchaguzi huo kwa asilimia 52 ya kura dhidi ya wagombea wengine 10 akiwemo mpinzani wake mkuu, kiongozi wa Chama cha Wananchi (CCC) Nelson Chamisa aliyepata asilimia 44 ya kura.
Chamisa amesema upinzani utaunda serikali mpya, na kusisitiza kuwa,“Hatutasubiri kwa miaka mitano. Lazima kuwe na mabadiliko sasa."