Mgombea wa chama kikuu cha upinzani katika uchaguzi wa rais nchini Zimbabwe, Nelson Chamisa amesema zoezi hilo la jana limekumbwa na kasoro nyingi na udanganyifu mkubwa, na kuna njama za kuchakachua matokeo ya uchaguzi huo.
Chamisa amesema licha ya mizengwe kugubika zoezi hilo la kidemokrasia, lakini ana uhakika kwamba ushindi utakuwa wao. Amesema, "Kuna njama za kutupokonya ushindi, lakini tutaendelea kushinikiza kutolewa matokeo halali na yenye itibari ya uchaguzi huu."
Wananchi wa Zimbabwe waliotimiza masharti ya kupiga kura, mapema jana Jumatano walilekea katika vituo vya kupigia kura kushiriki uchaguzi utakaoamua iwapo Rais wa sasa Emmerson Mnangagwa atashinda muhula wake wa pili na wa mwisho au la.
Kuna wagombea 11 wa urais katika uchaguzi huo, ingawaje mchuano mkali unatazamiwa kuwa baina ya Rais Mnangagwa anayewania kupitia chama tawala ZANU-PF na Nelson Chamisa wa Muungano wa Wananchi kwa ajili ya Mabadiliko (CCC).
Rais wa Zimbabwe mwenye umri wa miaka 80, alitoa wito kwa wananchi kutojihusisha na vurugu kabla, wakati na baada ya uchaguzi wa jana. Chamisa mwenye miaka 45, alishindwa kwa mwanya mdogo na Mnangagwa katika uchaguzi wa rais uliopita, mwaka 2018. Wagombea wakuu wa urais Zimbabwe, Rais Mnangagwa (Kulia) na Chamisa
Kamisheni ya Uchaguzi Zimbabwe (ZEC) imesema matokeo rasmi na ya mwisho ya uchaguzi huo yatatangazwa katika kipindi cha siku tano zijazo, lakini matokeo ya muda yataanza kutangazwa muda si mrefu.
Wakati huohuo, Andrew Makoni, Mwenyekiti wa asasi ya kiraia ya 'Zimbabwe Election Support Network' amesema uchaguzi wa mwaka huu una tofauti kubwa na wa 2018, kwa kuwa karatasi na suhula nyingine za kupigia kura hazikufikishwa vituoni kwa wakati.