Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Antonio Guterres amesifu hatua ya kusitisha vita katika eneo la Tigray nchini Ethiopia, wakati wa ziara yake ya kwanza tangu vita kati ya wanajeshi na wapiganaji wa Tigray vilipoanza miaka miwili iliyopita.
Guterres amesema kwamba Umoja wa mataifa unaednelea kuongeza msaada wa kibinadamu nchini humo ili kutosheleza mahitaji yanayohitajika kwa haraka.
Alikuwa akizungumza akiwa pamoja na mjumbe wa umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat.
Ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuendelea kuisaidia Ethiopia baada ya kusaini mkataba wa kusitisha vita mwezi uliopita.
Wizara ya fedha ya Ethiopia imesema kwamba itagharimu dola bilioni 20 kujenga upya miundo msingi iliyoharibiwa wakati wa vita hivyo vya miaka miwili.
Wafadhili wakuu wa Ethiopia ambao ni Marekani na Umoja wa ulaya walisitisha msaada wao kutokana na ripoti za ukandamizaji wa haki za kibinadamu.