Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ukuaji wa uchumi Tanzania ‘wamkuna’ Balozi wa Nigeria

A90502222ce82ec1d7235d9642138923 Ukuaji wa uchumi Tanzania ‘wamkuna’ Balozi wa Nigeria

Sun, 18 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

BALOZI wa Nigeria aliyemaliza muda wake wa utumishi nchini, Dk Sahabi Isa Gada (pichani) ameshukuru serikali ya Tanzania kwa ushirikiano aliopata wakati wote alipokuwa akitekeleza majukumu yake.

Dk Gada alisema akiwa nchini, ameona uchumi wa Tanzania ukikua kila wakati jambo ambalo ni zuri katika Afrika.

Alisema hayo jana katika mazungumzo kati yake na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Wilbert Ibuge, yaliyofanyika ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam baada ya kwenda kuaga.

Gada aliahidi kuwa ushirikiano uliopo utaendelezwa hasa ikizingatiwa kuwa Nigeria na Tanzania zimekuwa na uhusiano mzuri na imara tangu miaka ya 1962.

“Nimekuja kumuaga Katibu Mkuu kama ishara ya ushirikiano wetu kati ya Nigeria na Tanzania kwa kweli nashukuru sana kwa ushirikiano nilioupata wakati wa utumishi wangu hapa nchini.

“Nikiwa hapa nimeona uchumi wa Tanzania ukikua kila wakati jambo ambalo ni zuri hapa kwetu Afrika, pia namshukuru Katibu Mkuu, Wilbert Ibuge kwa kuuendeleza ushirikiano wetu kwa kweli naiona Tanzania kama nyumbani kwangu pia,” alisema.

Balozi Ibuge alisema kuwa Nigeria imekuwa na uhusiano mzuri wa kidiplomasia na Tanzania hasa katika kuunga mkono jitihada za kuimarisha sekta mbalimbali nchini ikiwemo sekta za usafirishaji, utalii, biashara na uwekezaji na usafirishaji

“Leo nimekutana na kufanya mazungumzo na Balozi Gada ambaye amemaliza muda wake wa utumishi hapa nchini na anarudi Nigeria, na kwa hakika mazungumzo marefu na yamelenga urafiki baina ya nchi zetu mbili na watu wetu pamoja na ushirikiano uliopo wa kibiashara, kibenki lakini pia tumezungumzia namna ambavyo Nigeria inapiga hatua kama Tanzania inavyopiga hatua,” alisema.

Ibuge aliendelea: “Mfano mzuri ni kuwa Nigeria ilipojenga mji wake mkuu mpya (Abuja) walikuja Tanzania kuja kujifunza na kupata ramani ya Dodoma ambayo wamemaliza kuijenga na sisi sasa tunaendelea kuijenga Dodoma tangu tulipotangaza rasmi kuhamia Dodoma mwaka 1973.”

Alimhakikishia Balozi Gada kuwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Nigeria utaendelea kuimarika ikiwa ni ishara ya kuwaenzi waasisi wa mataifa hayo; Mwalimu Julius Nyerere pamoja na Rais wa kwanza wa Nigeria, Nnamdi Azikiwe ambao walikuwa ni sehemu ya juhudi za kukomboa bara la Afrika na pia kusimi mwa Afrika.

Balozi Ibuge amesisitiza kuwa Tanzania na Nigeria zitaendelea kushirikiana katika sekta ya uwekezaji na biashara kwa maslahi mapana ya mataifa yote mawili. Aliwataka wafanyabiashara kutoka nchi hiyo kuwekeza nchini katika sekta za benki na utalii.

Chanzo: habarileo.co.tz