Kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga amesema ataongoza maandamano ya umma ya siku 14 iwapo Serikali haitapunguza makali ya gharama za maisha.
Odinga amesema atafanya hivyo kutokana na serikali kuondolea ruzuku ya chakula na elimu wakati wa janga la ukame na hivyo kuwa ni ishara ya Serikali kutojali maslahi ya wananchi.
Amesema, ”Lazima ruzuku irejeshwe na gharama ya bidhaa na kodi lazima zipunguzwe katika siku 14 zijazo, la sivyo tutaingia mtaani kwa maandamano kupinga hili.”
Hata hivyo, Rais wa Kenya William Ruto amekejeli mpango huo na kusema nchi inaongozwa kwa sheria na kwamba hataruhusu wala kuvumilia kuvunjwa kwa taratibu.