Wajumbe kutoka Jumuiya ya Afrika Magharibi, ECOWAS wameanza mazungumzo ya kutatua mzozo wa kisiasa nchini Niger kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa madarakani Rais Mohamed Bazoum wiki iliyopita.
Rais wa Nigeria na mkuu wa jumuiya ya kikanda, Bola Tinubu alikuwa amewapa wajumbe jukumu la kuhakikisha "azimio la kirafiki" linafikiwa walipokuwa wakianzisha mazungumzo nchini Niger na maeneo mengine ya kanda.
Ujumbe mmoja unaoongozwa na mkuu wa zamani wa jeshi la Nigeria, Jenerali Abdulsalami Abubakar unakutana na viongozi wa mapinduzi huko Niamey, mji mkuu wa Niger.
Ujumbe wa pili unaongozwa na Balozi Baba Gana Kingibe, mwanadiplomasia wa Nigeria na Katibu wa zamani wa Serikali unatarajiwa kuzungumza na viongozi wa Libya na Algeria.
Marekani pia imetoa wito wa kutafuta upatanishi wa amani nchini Niger.
"Kwa sasa, tunaangazia diplomasia, tunaamini bado kuna nafasi ya kufikia hilo," msemaji wa Katibu wa Kitaifa wa White House, John Kirby aliambia mkutano mfupi, Alhamisi.
ECOWAS ilikuwa imetoa msururu wa vikwazo, ikiwa ni pamoja na makataa ya siku 7 kulitaka jeshi nchini Niger kumrejesha madarakani Rais Bazoum aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia, ambaye bado anashikiliwa na utawala huo.
Ijumaa, Wakuu wa Ulinzi wa Afrika Magharibi Ijumaa, watahitimisha mkutano wa siku 3 huko Abuja, Nigeria ambapo majadiliano juu ya uwezekano wa kuingilia kijeshi yatafanyika, ikiwa diplomasia itashindwa.