Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ujirani mwema Tanzania, Burundi waridhishwa na usalama

621378153c3cd1dbdea7b98fe3f10caf Ujirani mwema Tanzania, Burundi waridhishwa na usalama

Sat, 5 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAJUMBE wa kikao cha ujirani mwema kati ya Tanzania na Burundi wameridhishwa na hali ya ulinzi na usalama mpakani, wakisema vikao hivyo vimesaidia kudhibiti matumizi ya silaha na ujambazi uliokuwa unasumbua raia.

Akizungumza kwenye kikao hicho kilichofanyika jana mjini Kigoma, Spika Mstaafu wa Bunge la Seneti la Burundi, Revelien Ndikuriyo alisema vikao vimewezesha kujadili kwa kina sababu za hali mbaya ya ulinzi na usalama na hatua madhubuti zimechukuliwa.

Ndikuriyo alisema hali kwa sasa ni shwari na wananchi wako huru kufanya shughuli za kiuchumi. “Mpaka wa Tanzania na Burundi uko salama na hakuna vitendo vya uhalifu na matumizi ya silaha kama ilivyokuwa awali,” alisema Spika mstaafu.

Aliongeza, “Hiyo inatokana na ushirikiano wa viongozi na wananchi wa nchi hizi mbili. Ni vizuri suala hili likafanywa pia kwenye mpaka na Congo ili kuimarisha ulinzi na usalama ambako vitendo vya ujambazi na uporaji bado vimekithiri.”

Ndikuriyo ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Makamba mstaafu nchini Burundi, alisema vikao hivyo vya ujirani mwema vimekuwa na manufaa makubwa katika kukuza ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi na utamaduni kutokana na mwingiliano wa karibu miongoni mwa wananchi wa Burundi na Tanzania.

Mkuu wa Mkoa wa Makamba, Ngozirazana Francose alisema masuala mbalimbali ya kijamii yanayohusu nchi hizo mbili yamekuwa na mafanikio makubwa katika kuyapatia ufumbuzi na ufafanuzi upande mmoja unapokuwa haaujaelewa au kuwapo malalamiko.

Alisisitiza vikao hivyo viwe chachu kupata suluhu masuala yanayojitokeza baina ya wananchi wa pande zote.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye alisema Tanzania na Burundi ni ndugu wanaogawanywa kwa mipaka iliyowekwa na wakoloni. Alisisitiza ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kijamii uimarishwe.

Andengenye alisema kuwa vikao hivyo vimesaidia kuimarisha ulinzi na usalama mipakani katika nchi hizo mbili hususani katika suala la kudhibiti na kubadilishana wahalifu.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Marco Gaguti alisema kuwa kwa sasa suala la usalama halizungumzwi kwa sababu kazi kubwa imefanywa katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu.

“Kazi kubwa imefanywa katika kushughulikia suala la ulinzi na usalama katika maeneo ya mikoa ya magharibi inayopakana na Burundi kwa sasa hakuna wahalifu labda mmoja mmoja wanaovizia, nao wakifanya kazi kubwa inafanywa kuwasaka,” alisema Gaguti.

Gaguti alisema wananchi wamejikita kushughulikia masuala ya kuiuchumi na biashara ambayo yaliathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na hali duni ya ulinzi na usalama iliyokuwapo.

Chanzo: habarileo.co.tz