Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ujenzi mtandao wa barabara EAC wazidi kupamba moto

3fc18f6586ecd1e7b792fc166b1b8d5d Ujenzi mtandao wa barabara EAC wazidi kupamba moto

Tue, 26 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

UJENZI wa mtandao wa barabara za lami kuziunganisha nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) unazidi kupamba moto baada ya kukamilika upembuzi yakinifu wa mradi wa ujenzi wa barabara ya kimataifa ya Tanzania -Uganda.

Barabara hiyo ambayo ujenzi wake utaanza hivi karibuni utayaunganisha maeneo ya Masaka - Kyotera – Mutukula-Mutukula - Kyaka na Bugene na Kasulo – Kumunazi.

Wakati barabara hiyo ikiwa katika hatua ya upembuzi, mtandao mwingine wa barabara inayounganisha Tanzania na Kenya ikipita katika maeneo ya Malindi - Lunga Lunga na Tanga - Bagamoyo ujenzi wake umepata ufadhili wa dola za Marekani milioni 322, huku barabara ya Nyakanazi - Kasulu - Manyovu nchini Tanzania ikikamilika.

Upembuzi yakinifu na ubunifu kwa ajili ya ujenzi wa barabara iitakayounganisha Tanzania na Uganda unafadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) chini ya kituo cha NEPAD-IPPF.

Taarifa iliyotolewa jana na Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha EAC ilieleza kuwa, upembuzi huo umefanywa na kampuni ya M / S LEA International Limited kutoka nchini Canada kwa kushirikiana na LEA Associates Asia Pvt Ltd kutoka India.

Taarifa hiyo ilisema katika barabara hiyo zitajenga kilomita 89.5 za sehemu ya barabara ya Masaka hadi Mutukula nchini Uganda, huku sehemu ya kilomita 30 kutoka Mutukula hadi Kyaka itaunganishwa na sehemu ya Tanzania ya kilomita 133 kutoka Bugene hadi Kumunazi kupitia Kasulo.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi ripoti ya muundo wa barabara hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa EAC anayeshughulikia mipango na miundombinu, Steven Mlote aliishukuru AfDB kwa msaada wa kifedha ambao umeiwezesha EAC kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa mradi huo wa mamilioni ya dola kati ya Uganda na Tanzania.

Alisema lengo la mtandao wa barabara za kimataifa ni kuwezesha maendeleo ya soko la kikanda la usafirishaji kupitia barabara katika eneo la Afrika Mashariki.

Mlote alisema Sekretarieti ya EAC sasa itajikita katika kutafuta fedha za ujenzi wa barabara hiyo, pamoja na kushirikiana na jumuiya nyingine za kikanda barani Afrika na ulimwengu kuboresha huduma za usalama barabarani.

Afisa huyo wa EAC pia alieleza muundo wa kina wa barabara ya Malindi - Lunga Lunga na Tanga - Bagamoyo kati ya Kenya na Tanzania kuwa umekamilika na AfDB imekubali kufadhili mradi huo kwa gharama ya dola za Marekani milioni 322.

“Kwa kuongezea, muundo wa kina wa barabara ya Nyakanazi - Kasulu - Manyovu nchini Tanzania ambayo inaunganisha barabara ya Rumonge - Bujumbura ya kilometa 78 nchini Burundi na barabara ya Lusahunga - Rusumo ya kilomita 92 nchini Tanzania inayounganisha na barabara ya Kayonza - Kigali ya kilometa 70 nchini Rwanda pia umekamilika,” alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz