Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uhusiano baina Rwanda, Burundi waanza kurejea

1a0b3edc4cd07fa3f3a997a3153b7553 Uhusiano baina Rwanda, Burundi waanza kurejea

Tue, 1 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

RWANDA na Burundi zimeanza kuonesha mwanga wa kurejesha mahusiano yao ya kisiasa, kutokana na viongozi wakuu wa masuala ya usalama kufanya mikutano katika mpaka wa Nemba na kuondoa tofauti zao.

Hii ni mara ya kwanza kwa viongozi wa pande hizo mbili, kukutana ana kwa ana kwa ajili ya kujadili namna ya kuimarisha mahusiano. Tofauti baina ya nchi hizo mbili jirani, zilianza mwaka 2015.

Mkuu wa Ulinzi wa Kiintelejensia wa Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF), Brigedia Jenerali Vincent Nyakarundi, aliongoza ujumbe wa nchi hiyo na Mkuu wa Majeshi wa Burundi, Kanali Ernest Musaba

aliongoza ujumbe wa nchi yake.

Mkutano huo wa ndani uliochukua saa nane kuanzia saa 9:00 asubuhi mpaka saa 4:00 jioni, ulitoa nafasi kwa kila nchi kueleza hali ya usalama.

Mkutano huo uliongozwa na Kamanda wa Kamati ya Pamoja (EJVM), Kanali Leon Mahoungou.

“Nina furaha kwa maamuzi yaliyofikiwa mwisho wa majadiliano haya na nimeridhishwa na jinsi mlivyo na dhamira ya kurejesha usalama kwenye mipaka yenu,” alisema.

Mahoungou alisema nchi hizo mbili, zimekubaliana kurejesha usalama kwa majadiliano na mawasiliano ya mara kwa mara kati vyombo vya usalama.

“Nimebaini kuwa sasa viongozi wakuu wa nchi hizo watafanya mawasiliano na kujaribu kupata suluhisho la kurejesha mahusiano rasmi kama ilivyokuwa awali,” alisema.

Hata hivyo, hakuna makubaliano yaliyosainiwa baina ya pande hizo mbili, lakini kila nchi imejizatiti kuhakikisha uhusiano mwema unarejea, huku ICGLR ikiendelea kusimamia kuhakikisha kila upande unatimiza wajibu wake.

Muda mfupi baada ya mkutano huo, Jeshi la Ulinzi Rwanda lilitoa taarifa iliyoeleza ulikuwa wa mafanikio makubwa, kwani ulitoa fursa ya kujadiliana matatizo ya kiusalama baina yao, kutafuta suluhisho na kujenga uaminifu baina ya nchi hizo.

Wiki iliyopita, wakimbizi 500 wa Burundi waliwezeshwa kuondoka nchini Rwanda, jambo linaloonesha kuimarika kwa uhusiano baina ya mataifa hayo. Mamia ya wakimbizi wengine wa Burundi, wanatarajia kurudi nchini mwao wiki zijazo.

Habari za kurejea kwa uhusiano wa nchi hizo zilianza Juni mwaka huu, baada ya Burundi kufanya uchaguzi mkuu na kumchagua Rais mpya, Meja Jenerali Everiste Ndayishimiye na Serikali ya Rwanda kumpongeza kwa kuchaguliwa kwake.

Katika salamu hizo za pongezi, Rwanda ilisema ipo tayari kurejesha uhusiano baina ya nchi hizo, hatua iliyopongezwa na raia wa nchi hizo mbili katika mitandao ya kijamii.

Nchi hizo zenye kabila moja, utamaduni mmoja na lugha moja, zilikuwa nchi moja iliyofahamika kama Rwanda-Urundi, mji mkuu ukiwa Usumbura, yaani Bujumbura ya sasa, chini ya ukoloni wa Ubelgiji.

Lakini kuanzia mwaka 2015 nchi hizo ziliingia katika kipindi kigumu cha kushutumiana kuunga mkono makundi ya waasi, ambapo Burundi iliihusisha Rwanda na jaribio lililofeli la kutaka kumpindua Rais Pierre Nkurunziza, ambaye aliitangaza Rwanda kuwa adui mkubwa wa Burundi.

Rwanda kwa upande wake imekuwa ikiishutumu Burundi kuunga mkono makundi ya waasi, waliofanya mashambulio yaliyotikisa maeneo yaliyo karibu na mpaka wa Burundi miaka miwili iliyopita.

Chanzo: habarileo.co.tz