Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uhuru amtuliza Kalonzo

Kalonzoopiic Data Kalonzo Musyoka

Fri, 13 May 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Rais Uhuru Kenyatta amefanikiwa kumtuliza Kiongozi wa Chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka ili akubaliane na muungano wa Azimio la Umoja One Kenya.

Awali, Kalonzo aliugomea wito wa kufanyiwa usaili wa kamati ya uteuzi ili awe mgombea mwenza wa Azimio la Umoja kama walivyofanyiwa wengine. Hata hivyo, Uhuru ameweza kumshawishi dakika za mwisho.

Mbali na Uhuru ambaye ndiye mwenyekiti wa Baraza la Azimio la Umoja, kiongozi mwingine aliyehusika kumshawishi Kalonzo ni Mwenyekiti wa Kenya African National Union (Kanu), Gideon Moi.

Hata hivyo, Kalonzo alisema uamuzi wa kuitikia wito wa kamati ya uteuzi wa mgombea mwenza ulitokana na utashi wake binafsi na si ushawishi na kukiri kuwa kabla ya kuitikia wito huo alizungumza na Uhuru pamoja na Gideon.

Vyanzo vya habari ndani ya Azimio vimebainisha kuwa Uhuru alikuwa na hofu Kalonzo asingehudhuria mkutano wa usaili na kamati hiyo ingetuma ujumbe mbaya kwani kiongozi huyo wa Wiper alikuwepo siku ya uzinduzi wa Baraza la Azimio la Umoja.

Uzinduzi huo wa baraza ulifanyika kwa mkutano ulioongozwa na Uhuru ukiwa na wajumbe kutoka vyama vyote vya Azimio la Umoja One Kenya, waliamua kuundwa kwa kamati maalumu ya kuchakata maoni na mapendekezo ya kumpata mgombea mwenza.

“Mwenyekiti wa Kanu, Gideon Moi ambaye ndiye alimpendekeza Kalonzo kwenye kamati ili ateuliwe kuwa mgombea mwenza, ilibidi afanye kazi kubwa kumshawishi ahudhurie kikao cha usaili wa kamati, vinginevyo ingeonekana kuna agenda ya siri,” kilisema chanzo ndani ya Azimio.

Wiper cha Kalonzo, Kanu kinachoongozwa na Gideon, na vyama vingine kama Narc Kenya cha Martha Karua, Amani National Congress (ANC), cha Musalia Mudavadi na Pamoja African Alliance (PAA) chini ya Moses Wetang’ula, awali viliunda ushirikiano waliouita One Kenya Alliance (OKA).

Kanu, Wiper na Narc Kenya, ni vyama vya OKA vilivyojiunga na Azimio la Umoja hivyo kutengeneza muungano mpana wa Azimio la Umoja One Kenya. ANC na PAA, wao waliichagua Kenya Kwanza.

Mgombea urais wa Azimio la Umoja One Kenya ni Kiongozi wa Orange Democratic Movement (ODM), Raila Odinga wakati mbeba bendera wa Kenya Kwanza ni bosi wa United Democratic Alliance (UDA), William Ruto.

Katika upande mwingine, Gideon ni mmoja wa majina yaliyovuka mchujo wa awali kumpata mgombea mwenza, ambaye aliitwa kwenye usaili na alihudhuria.

Baada ya kumaliza usaili, katibu wa habari wa Gideon, Joseph Towett, alitoa taarifa kwa umma akisema: “Gideon anatoa shukurani za kipekee kwa kamati adhimu inayoundwa na watu makini kwa kumfikiria na yeye kuwa anaweza kuwa mgombea mwenza wa Azimio la Umoja, ila msimamo wangu ni uleule, nataka mheshimiwa Kalonzo Musyoka ndiye apewe nafasi hiyo.”

Akizungumza na vyombo vya habari baada ya kumaliza usaili, Kalonzo alisema uamuzi wake wa kuitikia wito wa kamati ni kudhibiti jaribio lolote la kutumia kutotokea kwake kwenye mkutano huo kama kigezo cha kumnyima fursa ya kuwa mgombea mwenza.

“Nataka niwaambie kuwa uamuzi wa kuja kwenye kamati ni wangu kwa sababu niligundua lazima tusiruhusu watu wapate sababu ya kusema aligoma kuja kwenye kamati,” alisema Kalonzo ambaye ni miongoni mwa wanasiasa wenye ushawishi na siasa za Kenya.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz