Mhimili wa Mahakama Kenya umeendelea kuthibitisha kuwa wenyewe upo huru.
Machi 31, mwaka huu, Mahakama Kuu Kenya ilihitimisha kiu ya Rais Uhuru Kenyatta kufanya mabadiliko ya Katiba ili kuruhusu kuingizwa kwa mapendekezo 78 ya BBI.
BBI ni nini? Jibu litafuata! Kwanza ieleweke kuwa jopo la majaji saba, wakiongozwa na Jaji Mkuu wa Kenya, Martha Koome walitoa uamuzi kuwa Uhuru alikosea kwa kuanzisha mchakato wa mabadiliko ya Katiba.
Juni mwaka jana, ilitarajiwa mabadiliko ya kikatiba Kenya yangefanyika ili kuruhusu mapendekezo ya BBI kuingia.
Mei 13, mwaka jana, jopo la majaji watano Mahakama ya Juu Kenya, lilitoa hukumu yenye kueleza kuwa mchakato wa mabadiliko ya kikatiba ulikosewa.
Mahakama ilieleza kuwa Katiba ya Kenya imetoa milango miwili ya uanzishwaji wa mchakato wa mabadiliko ya kikatiba. Wa kwanza ni kupitia Bunge, pili ni maoni ya wananchi. Mchakato wa BBI ulikosewa kwa sababu uliasisiwa na kufanyiwa kampeni na Uhuru.
Advertisement Agosti 20, mwaka jana, majaji saba wa Mahakama ya Rufaa walitoa hukumu yenye kukazia uamuzi wa Mahakama ya Juu. Kisha, Mahakama ya Rufaa ikapendekeza Uhuru kushitakiwa kwa kuvunja Katiba kupitia mchakato wa BBI.
Halafu, Mahakama ya Kuu, ambayo ndiyo ya juu zaidi Kenya, chini ya Jaji Mkuu, iliendelea kukazia uamuzi kwamba, uanzishwaji wa mchakato wa mabadiliko ya katiba chini ya BBI ulikosewa, lakini ukatengua tafsiri ya kwamba Rais anaweza kushitakiwa.
BBI ni nini?
Ni Building Bridge Initiative (BBI), maana yake ni mpango wa kujenga daraja. Kila kitu kilianza Machi 2018, Uhuru na Kiongozi wa Upinzani, Raila Odinga waliposhikana mikono na kukubaliana kuanza mwanzo mpya wa kuijenga nchi yao bila migawanyiko ya kisiasa, ukabila na matabaka.
Machafuko au migogoro yenye kuibuka mara kwa mara vipindi vya uchaguzi ni sababu ya Uhuru na Raila kuketi, kama Wakenya, wenye kuipenda Kenya na kuitakia kesho njema, wakazungumza na kuzika tofauti zao, kisha kupata mawazo yaliyofanikisha ripoti ya BBI.
Baada ya mazungumzo ya Uhuru na Raila, kiliundwa kikosi kazi cha wajumbe 14, kikapewa ajenda tisa. Kikazunguka majimbo (counties) 47 ya Kenya ili kupata mawazo ya namna ambavyo Wakenya wangependa nchi yao iwe.
Katika ajenda tisa; ya kwanza ni jinsi ya kumaliza mgawanyiko wa kikabila. Pili, ushirikishwaji wa vyama vya upinzani katika muundo wa Serikali.
Tatu, jinsi ya kutatua misuguano ya uchaguzi; nne, ulinzi na usalama na tano ni namna ya kupambana na rushwa.
Sita ni jinsi ya kushughulikia ukosefu wa moyo wa utaifa kwa wananchi; saba, haki na uwajibikaji; nane, mgawanyo sawa wa matunda ya nchi na tisa ni kutanua nguvu ya mamlaka kwa wananchi na uwakilishi.
Ni ajenda hizo zilisababisha kikosi kazi cha BBI kije na mapendekezo ya mabadiliko ya vifungu vya Katiba ya Kenya ya mwaka 2010, pia vipo vilivyopendekezwa kufutwa, vingine kubadilishwa matamshi na kuna ambavyo vingeongezwa.
Uchambuzi
Kwanza ni pendekezo la kuwa na Rais wa muhula mmoja wa miaka saba, bila nyongeza. Ukurasa wa 19 wa ripoti ya BBI, utetezi wa hoja hiyo umetolewa kwa mifano dhahiri, kwa hakika inaeleweka na kuridhisha.
Wanataka Rais akiingia madarakani asiwe na nafasi ya kugombea muhula wa pili, kwamba kihistoria kila mara Rais aliye madarakani anapogombea muhula wa pili, ndipo migogoro na machafuko hutokea.
Wametoa mifano ya ghasia za uchaguzi mwaka 1991/92 na 1997 kipindi Daniel Moi alipokuwa akigombea kuongeza muhula wa uongozi, machafuko ya mwaka 2007/8 Mwai Kibaki alipogombea muhula wa pili, vilevile mivutano na uchaguzi kurudiwa mara mbili mwaka 2017, Uhuru alipogombea muhula wa pili.
Mifano mingine ni hali ya amani ilivyokuwa mwaka 2002 na 2013, wakati marais madarakani walipokuwa hawagombei. Ni kipimo kuwa marais madarakani husababisha ghasia kwa kutaka ushindi wa kufa au kupona.
Ipo hoja nyingine ya matumizi ya fedha, kwamba Rais madarakani anapokuwa anagombea kuongeza muhula wa uongozi, hujiwezesha kwa fedha za umma ili kugharimia uchaguzi.
Sababu ya msingi nyingine ni kuwa Rais anapokuwa na matarajio ya kuwania muhula wa pili, miaka miwili ya kwanza anapoingia madarakani huitumia kulipa fadhila kwa waliomsaidia na mitatu inayofuata hujifanyia maandalizi ya uchaguzi, hivyo muda wa kutoa huduma huwa mdogo.
BBI inataka Rais wa Kenya kutokuwa mtendaji, bali mkuu wa nchi mwenye wajibu wa kuliunganisha Taifa. Rais atateua Waziri Mkuu kutoka kwenye chama chenye wabunge wengi. Waziri Mkuu ndiye atakuwa Mkuu wa Serikali (mtendaji).
Hiyo ni tafsiri kuwa Kenya ilipendekezwa kuhama kutoka muundo wa Serikali ya urais (Presidential Model of Government) kama ilivyokuwa na kupewa mkazo na Katiba ya mwaka 2010, sasa inakaribisha Serikali ya Bunge (Parliamentary Democracy).
BBI inapendekeza Waziri Mkuu awe na manaibu watatu watakaoshirikiana kuendesha Serikali. Kati ya hao watatu, wawili ni kutoka vyama vya upinzani. Kwa maana hiyo, wanaoshinda na wanaoshindwa, wangeshirikiana kuihudumia nchi.
Kupitia BBI, Rais wa Kenya angechaguliwa kwa kura za majimbo kama Marekani. Hiyo ingesaidia kuondokana na hulka za kufanya kampeni za kikabila na kugawa watu. Mpinzani mkuu wa kiti cha urais anaposhindwa, moja kwa moja anakuwa mbunge ili aitumikie nchi yake.