Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uhuru, Museveni, Kagame walimlilia Magufuli

16e95186e7294fe26cd941b967b550ad Uhuru, Museveni, Kagame walimlilia Magufuli

Fri, 19 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta ameongoza wakuu wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo kutuma salamu za rambirambi kutokana na kifo cha Rais wa Tanzania, Dk John Magufuli.

Viongozi hao wametoa pole kwa familia ya Magufuli, Serikali ya Tanzania na Watanzania kwa ujumla. Rais Uhuru alituma salamu za rambirambi kwa mke wa Rais Magufuli, Mama Janet Magufuli, familia yake, serikali na wananchi wa Tanzania kwa kufiwa na mpendwa wao.

Rais Magufuli aliaga dunia juzi katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam, kutokana na maradhi ya moyo. Rais Uhuru alisema Bara la Afrika na dunia wamempoteza kiongozi ambaye maono na uongozi wake yameiwezesha Tanzania kupiga hatua kubwa kimaendeleo na ipa kuwezesha mshikamano katika nchi za EAC.

Aliamuru taifa lake kuomboleza kifo hicho kwa siku saba na bendera ya nchi yake kupepea nusu mlingoti mpaka Magufuli atakapozikwa, na pia aliamuru bendera ya EAC kupepea nusu mlingoti kwa wakati wote wa maombolezo.

“Nakumbuka kwa dhati mara nyingi tulikutana na kuongea kuhusu maendeleo ya nchi zetu mbili, nakumbuka safari yake rasmi ambayo alitutembelea hapa Kenya na kwa pamoja tukafungua barabara ambayo tunaiita Southern by Pass,” alisema Rais Uhuru.

Alisema Rais Magufuli alimpa heshima kubwa baada ya kusisitiza kuwa lazima amtembelee mama yake, Mama Ngina Kenyatta kumjulia hali. “Mimi pia alinialika nimtembelee kule kwake Chato na nikapata nafasi ya kumsalimia mama yake na kuongea naye.

Nililala nyumbani kwake na tukaongea mengi kuhusu nchi zetu mbili na Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ujumla,” aliongeza Rais huyo wa Kenya.

Alisema jana asubuhi alizungumza na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na kumpa salamu za pole kutoka kwa wananchi wa Kenya na kumhakikishia kuwa yeye na wananchi wa Kenya wamesimama naye wakati huu mgumu.

Rais wa Rwanda, Paul Kagame aliungana na viongozi wengine EAC kutuma salamu za rambirambi kwa serikali na familia ya Rais Magufuli. Katika ujumbe aliotuma kupitia akaunti yake ya Twitter, Kagame alisema, “Tumeshtushwa na taarifa za kufariki kwa kaka na rafiki yangu Rais John Magufuli.” Waziri Mkuu wa Rwanda, Edouard Ngirente alitangaza kuwa Rais Kagame ametangaza muda wa maombolezo utakaokwisha baada ya maziko ya Rais Magufuli.

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni katika ujumbe wake katika ukurasa wake wa Twitter alisema amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kufariki dunia kwa Rais Magufuli akisema alikuwa kiongozi wa mfano aliyepigania sio tu uchumi wa Tanzania, bali uchumi wa Afrika Mashariki.

Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye alisema amesikitishwa na taarifa za kifo cha rafiki na kaka yake Rais Magufuli. Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya na kiongozi wa upinzani, Raila Odinga katika salamu zake za rambirambi aliitaja, familia yake na ya Rais Magufuli kuwa zina ushirikiano wa muda mrefu.

Odinga alisema binafsi amekuwa akipitia magumu mengi katika safari yake ya kisiasa na mtu aliyekuwa akimpa faraja kubwa alikuwa Rais Magufuli. Rais wa Afrika Kusini, Cyirl Ramaphosa kupitia ukurasa wake wa tweeter aliandika kuwa Afrika Kusini inungana na Watanzania katika kuombeleza kifo cha Rais Magufuli.

“Nimezungumza na Makamu wa Rais Samia na kumpatia salamu zetu za rambirambi hasa katika kipindi hiki kigumu wanachopitia,” aliandika Ramaphosa.

Rais wa Namibia, Hage Geingob alisema Tanzania imepoteza kiongozi mzalendo huku Namibia ikipoteza rafiki na kaka. Rais wa Malawi, Lazarus Chakwera alisema amepokea kwa mshutuko na huzuni taarifa za kifo cha rafiki na kaka yake Rais Magufuli.

“Natoa salamu zangu za rambirambi kwa familia yake na watu wa Tanzania ambao tunatumia wote mpaka na urithi wetu,” alisema Rais Chakwera.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres alieleza kusikitishwa na taarifa za kifo cha Rais Magufuli, “Katibu Mkuu anatuma salamu za rambirambi kwa familia ya Rais, kwa Serikali na kwa watu wa Tanzania,” ilieleza taarifa ya Msemaji wa Katibu Mkuu wa UN, Stephane Dujarric.

Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa, Zlatan Miliši? kwa upande wake, alisema Umoja wa Mataifa Tanzania umehuzunishwa na kifo cha Rais Magufuli na unatoa pole kwa serikali, familia na watanzania wote.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Adhanom naye alituma salamu za rambirambi kwa Watanzania na serikali ya nchi hiyo kutokana na kifo cha Rais Magufuli.

Katibu Mtendaji wa Jumuiya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Dk Stergomena Tax alitoa salamu za rambirambi za jumuiya hiyo kutokana na msiba huo.

“Serikali ya Tanzania na SADC imepoteza kiongozi bora. Pole sana wote, pole Mama Janet na familia,” alisema. Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson alielezea kusikitishwa na kifo cha Rais Magufuli.

Viongozi wengine waliotuma salamu za rambirambi ni Balozi wa Uholanzi nchini Verheul Jeroen, Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa, Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro na Balozi wa Marekani nchini, Donald Wright.

Chanzo: www.habarileo.co.tz