Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uhasama DRC, Rwanda washika kasi

Rwanda Congo AU AU Uhasama DRC, Rwanda washika kasi

Sat, 11 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, limeituhumu Rwanda kushambulia kwa makombora shule moja nchini mwake na kuwaua watoto wawili huku ikidai kitendo hicho ni uhalifu wa kivita dhidi ya binadamu.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya Habari, Jeshi hilo limesema vikosi vya Rwanda vilianzisha mashambulizi ya mizinga wakati wa mchana Juni 10, 2022, katika maeneo mawili ya Rutshuru yaliyopo jimbo la Kivu Kaskazini, mashariki mwa DRC.

“Mabomu yalipiga shule na kuua wavulana wawili wa miaka sita na saba, na mvulana moja alijeruhiwa katika shambulio hilo na pia walilipua shule nzima kwa mabomu, sasa huu ni uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu,” ilisema taarifa hiyo.

Tuhuma hizi zinakuja muda mfupi tangu Wizara ya Ulinzi ya Rwanda jana Juni 10, 2022, kuishutumu DRC kurusha makombora mawili katika ardhi yake, hali inachochea kuzorota kwa uhusiano wa nchi hizo tangu kuzuka upya kwa wanamgambo wa M23 mashariki mwa DRC.

Hata hivyo, DRC inaishutumu Rwanda kwa kuunga mkono kundi la Watutsi wa Kongo, na mwezi uliopita ilisema imewazuia wanajeshi wawili wa Rwanda katika eneo lake la mashariki kama ushahidi, madai yanayokanushwa na Serikali ya Rwanda.

Jana Juni 10, 2022, jeshi la DRC nalo lilikanusha tuhuma zake toka Rwanda kwamba liliwarushia makombora na kudai Rwanda ilifanya shambulio katika ardhi yake kwa nia ya kupotosha jumuiya ya kimataifa.

“Madai ya Rwanda si ya kweli bali wamejishambulia wenyewe ili kuihadaa Jumuiya ya Kimataifa kwamba DRC ni mchokozi lakini habari hizi ni za uongo na zinalenga kutuvuruga haitakubalika,” ilisema taarifa ya DRC.

Uhusiano kati ya DRC na Rwanda umekuwa mbaya tangu kuwasili kwa Wahutu wa Rwanda mashariki mwa DRC, wanaotuhumiwa kuwachinja Watutsi wakati wa mauaji ya kimbari ya 1994 nchini Rwanda.

Hata hivyo, hali ilizidi kuwa mbaya baada ya Rais Felix Tshisekedi kushika madaraka 2019, ingawa kuzuka kwa ghasia za M23 kumeongeza hali ya wasiwasi, huku Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa wakitoa wito wa utulivu, licha ya mvutano wa kikanda.

DRC inatoa shutuma hizi huku ikiwa na ugeni wa Mfalme Philippe toka Ubelgiji, ambaye yupo nchini humo kwa ziara ya kihistoria ya siku sita katika koloni lake hilo la zamani, na imeratibiwa kuwa atazuru mji wa Bukavu siku kesho Juni 12, 2022.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live