Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ugonjwa mpya wa kisonono wagunduliwa Nairobi

Ugonjwa Mpya Wa Kisonono Wagunduliwa Nairobi Ugonjwa mpya wa kisonono wagunduliwa Nairobi

Thu, 12 Jan 2023 Chanzo: Bbc

Watafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Matibabu ya Kenya (Kemri) wanasema aina mpya ya ugonjwa wa kisonono, ugonjwa wa zinaa unaostahimili viuavijasumu vya kawaida, unasambaa katika mji mkuu, Nairobi, hasa miongoni mwa wafanyabiashara wa ngono wa kike.

Waliohusika na utafiti huo wanalaumu taarifa potofu kwani baadhi ya wafanyabiashara ya ngono, ambao wanatumia tembe za kila siku za kuzuia VVU, wanaamini kuwa zitawaepusha na magonjwa ya zinaa na hawakuweza kujadiliana kuhusu matumizi ya kondomu.

Zaidi ya wafanyabiashara 350 wa ngono kutoka zahanati moja jijini Nairobi, ambayo iliripoti visa vingi vya ugonjwa wa kisonono, walishiriki katika utafiti huo.

Robo tatu ya washiriki walikiri kufanya mapenzi bila kinga na wapenzi wao na wateja - kwani inalipa zaidi. Baadhi yao walisema walilala na angalau wateja 29 katika wiki mbili.

Watafiti hao wanaitaka serikali ya Kenya kubadilisha sera ya sasa ya matibabu pamoja na kutetea uchunguzi zaidi ili kubaini jinsi tatizo hilo limeenea nchini.

Kisonono ni mojawapo ya magonjwa ya zinaa yanayoenea zaidi duniani. Zaidi ya kesi milioni 80 huripotiwa ulimwenguni kila mwaka.

Gonorrhoea/Kisonono ni nini?

·Ugonjwa huu husababishwa na bakteria aitwaye Neisseria gonorrhoeae.

·Maambukizi huenezwa na ngono, mdomo na sehemu ya nyuma bila kinga.

·Kati ya walioambukizwa, takriban mmoja kati ya wanaume 10 wanaoshiriki mapenzi ya jinsia tofauti na zaidi ya robo tatu ya wanawake, na wanaume wa mapenzi ya jinsia moja , hawana daalili zinazoweza kutambulika kwa urahisi.

·Lakini daalili zinaweza kujumuisha kutokwa na uchafu mwingi wa kijani kibichi au manjano kutoka sehemu za siri, maumivu wakati wa kukojoa na kutokwa na damu kati ya hedhi.

·Maambukizi yasiyotibiwa yanaweza kusababisha utasa, ugonjwa wa uvimbe wa pelvic na inaweza kupitishwa kwa mtoto wakati wa ujauzito.

Chanzo: Bbc