Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uganda yawahakikishia usalama watalii baada ya shambulio

Utalii Kinara Kenya Uganda yawahakikishia usalama watalii baada ya shambulio

Thu, 19 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali ya Uganda kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (UWA) imewahakikishia watalii usalama wao kufuatia shambulio la kigaidi la Jumanne jioni lililopelekea watalii wawili wa kigeni na mwongozaji wao mmoja raia wa Uganda kuuawa karibu na Mbuga ya Kitaifa ya magharibi mwa nchi hiyo.

Kwenye taarifa yake, Mamlaka ya Usimamiaji wa Wanyamapori nchini Uganda (UWA) imesema: "Watu wasiojulikana" walivamia gari la watalii hao na kulichoma moto kwenye eneo la Nyamunuka, kando ya Barabara ya Katwe inayoelekea kwenye mbuga hiyo ya taifa ya magharibi mwa Uganda.

Mamlaka hiyo imeongeza kuwa, inafanya kazi kwa bidii ili kubaini shambulio hilo limetokea katika mazingira gani na hatua gani zinapaswa kuchukuliwa kuwahakikishia watalii usalama wao.

Taarifa hiyo aidha imesema: "Usalama wa watalii wanaotembelea maeneo yetu ya hifadhi ni muhimu sana kwetu. Hifadhi zetu zote ziko wazi kwa ajili ya kupokea wageni, na tunaendelea kushirikiana na vyombo vingine vya usalama ili kuhakikisha kuwa watu wote wanaotembelea hifadhi zetu wanakuwa salama." Utalii ni katika sekta inayoiingizia Uganda pato jingi la kigeni

Jeshi la Polisi ya Uganda linawashutumu waasi wa Allied Democratic Forces (ADF) kuwa ndio waliofanya shambulio hilo kutokea nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Taarifa ya jeshi hilo imesema kuwa, majeshi ya Uganda kwa kushirikiana na yale ya DRC yanaendeleza msako dhidi ya waasi hao wa ADF.

Ijumaa iliyopita pia, waasi wa ADF walichoma moto trela la lori moja la raia na kuua kwa uchache mtu mmoja katika shambulio la kuvizia la barabarani huko Kasese, yapata kilomita mbili kutoka mpaka wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Mwezi Juni mwaka huu pia, waasi wa ADF walishambulia shule moja hukohuko Kasese na kuua zaidi ya watu 40.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live