Jana Jumanne, Uganda iliungana na nchi nyingine za Afrika kuadhimisha Siku ya Kupambana na Ufisadi barani humo, huku serikali ikitoa mwito kwa wananchi wote wa Uganda kuisaidia serikali kupambana na rushwa, tabia mbaya ambayo inasababisha hasara kubwa kwa hazina ya serikali.
Uganda inapoteza kwa uchache dola bilioni 2.7 kwa mwaka kutokana na ufisadi, ambayo ni sawa na asilimia 23 ya bajeti ya kila mwaka ya serikali. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya jana Jumanne iliyotolewa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Beti Kamya, ambaye pia ni mkuu wa taasisi ya kupambana na ufisadi ya serikali ya Uganda.
Mkaguzi Mkuu huyo wa Hesabu za Serikalli ya Uganda amesema, hatua zimechukuliwa za kuwatia mbaroni wanaohusika na ufisadi. Jumla ya kesi 375 za rushwa zilifuatiliwa na uchunguzi wake kukamilika katika ngazi za Serikali za Mitaa kuanzia mwezi Julai hadi Desemba 2022. Maandamano ya kupinga ufisadi nchini Uganda
Ameongeza kuwa, taasisi yake ya kupambana na ufisadi ilifanikiwa kurejesha serikali dola 600,000 kutoka kwa wale waliopatikana na hatia ya ufisadi kufikia mwezi Desemba 2022. Hata hivyo amekiri kwamba kiwango hicho ni kidogo sana kwani kiwango kilichokusudiwa kufikiwa kilikuwa ni dola milioni 9.
Kamya amesema serikali peke yake haiwezi kufikia malengo yanayokusudiwa hivyo amewataka wananchi wote wa Uganda kushirikiana na serikali kupiga vita rushwa kwa kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu gharama na madhara makubwa ya rushwa kwa taifa. Amesema, rushwa ni uvundo ambao kila mwananchi anapoaswa kuuchukia mno.
Mkaguzi Mkuu huyo wa Hesabu za Serikali ya Uganda pia amesema, Umoja wa Afrika AU unakadiria kuwa bara hilo hupoteza dola za bilioni 140 kwa ufisadi kila mwaka.