Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uganda yashinikiza kuharamishwa kwa mashirika ya wapenzi wa jinsia moja

Uganda Yashinikiza Kuharamishwa Kwa Mashirika Ya Wapenzi Wa Jinsia Moja Uganda yashinikiza kuharamishwa kwa mashirika ya wapenzi wa jinsia moja

Mon, 13 Feb 2023 Chanzo: Bbc

Mamlaka nchini Uganda zinatoa wito wa kuharamishwa kwa mashirika ya wapenzi wa jinsia moja LGBTQ, na shughuli zao nchini humo.

Ripoti ya Januari kutoka Ofisi ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, chombo rasmi ambacho kinasimamia kazi za mashirika hayo, inataka marekebisho ya sheria za nchi ili kuharamisha shughuli za LGBTQ.

Katika njia mbadala inahimiza kupitishwa kwa sheria mpya "inayopiga marufuku uendelezaji wa shughuli za LGBTQ nchini".

Inasema serikali inahitaji kutoa rasilimali zaidi kwa Ofisi ya Mashirika yasiyo ya kiserikali ili iweze "kutambua na kuwaondoa wale wanaohusika katika shughuli ambazo zinaathiri maslahi ya watu wa Uganda".

Mahusiano ya wapenzi wa jinsia moja yameharamishwa nchini Uganda, na mtu anaweza kuhukumiwa hadi kifungo cha maisha kwa "makosa yanayoenda kinyume na maumbile".

Rpoti hiyo ni matokeo ya uchunguzi wa mwaka mzima wa shughuli za mashirika yasiyo ya kiserikali yanayojihusisha na kazi za haki za kingono za watu walio wachache nchini i Uganda.

Ofisi hiyo inasema ilipokea malalamishi dhidi ya mashirika mbalimbali, lakini haikueleza chanzo cha malalmishi hayo.

Kwa jumla mashirika 26 yasiyo ya kiserikali yalichunguzwa lakini uchunguzi bado haujahitimisha kazi yake.

Inasema kuwa Sexual Minorities Uganda, mojawapo ya mashirika mashuhuri ya ya LGBTQ nchini humo, haikusajiliwa rasmi kama shirika lisilo la kiserikali au la kibiashara.

Mamlaka inayosimamamia mashirika hayo iliamuru kufungwa kwa shirika hilo mnamo Agosti 2022, lakini shirika hilo tangu wakati huo limewasilisha kesi katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki kupinga kufungwa kwake.

Maombi ya usajili ya angalau mashirika mengine matatu kwa ofisi yalikataliwa kutokana na kuhusika kwao katika kazi ya haki za binadamu ya wapenzi wa jinsia moja.

Katika wiki za hivi karibuni, maafisa kadhaa wa serikali na viongozi nchini wamekuwa wakishtumu mashirika hayo kwa "kukuza shughuli za wapenzi wa jinsia moja" nchini.

Wiki iliyopita, Askofu Mkuu Stephen Kaziimba, mkuu wa Kanisa la Kianglikana la Uganda, alikosoa uamuzi wa hivi karibuni wa Kanisa la Uingereza kubariki ndoa za watu wa jinsia moja.

Askofu Mkuu Kaziimba alisema kuwa mapenzi ya jinsia moja ni dhambi na kwamba kanisa la Kianglikana nchini Uganda halitaunga mkono jambo hilo.

Pia wito umetolewa upya bungeni kutaka mswada mpya wa kupinga uhusiano wa kimapenzi wa aina hiyo uwasilishwe kwa mjadala.

Uganda ilielekezewa darubini kimataifa ilipopitisha sheria ya kupinga mapezi ya jinsia moja mwaka 2013.

Baadaye ilibatilisha sheria hiyo mwaka wa 2014 pale mahakama ilipoamua kuwa ilipitishwa bila akidi inayotakiwa bungeni.

Chanzo: Bbc