Uganda na Saudi Arabia zimerejelea upya makubaliano ya kibiashara ambayo yanaruhusu kuanza tena usafirishaji wa wafanyikazi katika nchi hiyo ya ghuba.
Makubaliano hayo yalisitishwa mwezi Disemba mwaka jana kufuatia madai ya unyanyasaji na kuteswa kwa wafanyakazi wahamiaji wa Uganda.
Baadhi ya wahamiaji wa Uganda waliripotiwa kujiua kwa madai ya kudhulumiwa nchini Saudi Arabia.
Waziri wa Leba wa Uganda Betty Amongi alisema siku ya Alhamisi kwamba serikali zote mbili zimekubaliana kulinda haki za wafanyakazi wahamiaji.
Katika makubaliano hayo mapya, waajiri wa Saudi Arabia hawatakata tena mishahara kwa upande mmoja na wafanyakazi wa Uganda watakimbilia mamlaka husika endapo kutazuka migogoro ya kimkataba.
Nchi zote mbili pia zitaanzisha utaratibu wa kutatua masuala ya ustawi na haki za wafanyakazi wa ndani.
"Pande zote mbili zinapaswa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waajiri na mashirika ya kuajiri kwa ukiukaji wowote wa sheria, kanuni katika nchi zote mbili," Bi Amongi alisema.
Takriban Waganda 150,000 wanaishi na kufanya kazi nchini Saudi Arabia na wengi wao wakifanya kazi za ndani, kulingana na vyombo vya habari vya nchini humo.