Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uganda wazima ndoto za Kili Stars Chalenji

88948 Kill+pic Uganda wazima ndoto za Kili Stars Chalenji

Wed, 18 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

WENYEJI timu ya Taifa ya Uganda, imeibuka na ushindi wa bao 1-0, dhidi ya Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars' katika mchezo wa nusu fainali wa mashindano ya Chalenji uliopigwa Uwanja wa KCCA, Uganda jioni ya leo Jumanne. Bao lililozima ndoto za Tanzania Bara, lilifungwa dakika ya 85 na Fahad Bayo na kupeleka shangwe na furaha kwa wachezaji, ndugu na jamaa zake waliokuwa wamefurika ndani na nje ya uwanja huo kutoka sehemu mbalimbali za Uganda na sasa wanasubiri mchezo wa fainali. Awali katika dakika 45 za kipindi cha kwanza, safu ya ulinzi ilikuwa na changamoto kubwa kutokana na kuandamwa na washambuliaji wa Uganda. Mabeki wa Stars, walifanya makosa ya mara kwa mara katika kipindi cha kwanza ambacho kilimalizika kwa sare tasa ambayo kama wenyeji wangeyatumia vizuri, wangekwenda mapumziko wakiongoza. Makosa hayo ni kukosa mawasiliano, udhaifu katika ukabaji pamoja na kupoteza mipira kizembe ambayo mara kadhaa yameliweka lango la Stars katika wakati mgumu. Mfano wa makosa hayo ni lile la dakika ya 29, beki Bakari Mwamnyeto alipiga pasi mkaa iliyonaswa na Uganda, kisha wakapasiana harakaharaka na kumkuta Bright Anukani ambaye alipiga shuti lililopaa na kushindwa kuiandikia bao timu yake. Ndani ya dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza, Mwamnyeto tena alipiga pasi hafifu iliyonaswa na Fahad Bayo ambaye alimtengea Allan Okello vizuri lakini akapiga shuti likapaa juu na kutoka nje. Uganda wameonekana kutumia vyema makosa ya Kilimanjaro Stars ya kukatika kwa safu ya kiungo na ulinzi jambo lililosababisha wapeleke mashambulizi ya mara kwa mara langoni mwa wageni hao kutoka Dar es Salaam. Pamoja na washambuliaji wa Stars kutopata huduma sahihi kutoka kwa viungo wake, mara kadhaa walijaribu kuliweka majaribuni lango la Uganda lakini safu ya ulinzi ya wapinzani chini ya kipa, Charles Lukwago na beki, John Revita ilikuwa makini kuondosha hatari hizo. Miongoni mwa mashambulizi hatari ambayo ukuta wa Uganda uliyafanyia kazi vizuri ni lile la dakika ya nyongeza ya kipindi cha kwanza ambapo Eliuter Mpepo alipokea pasi nzuri ya Juma Abdul na kupiga shuti ambalo liliokolewa kwa ustadi na Lukwago ikawa kona isiyozaa matunda. Dakika ya 38, Stars ilipata pigo baada ya kipa wake, Aishi Manula kuumia na nafasi yake ilichukuliwa na Metacha Mnata. Pia, kKatika kipindi hicho cha kwanza, Jonas Mkude alionyeshwa kadi ya njano kwa kumchezea madhambi, Bright Anukani.

VIKOSI TANZANIA BARA Aishi Manula, Juma Abdul, Gadiel Michael, Bakari Mwamnyeto, Kelvin Yondani, Jonas Mkude, Hassan Dilunga, Mzamiru Yassin, Ditram Nchimbi, Eliuter Mpepo, Nickson Kibabage.

UGANDA Lukwago Charles, Mustafa Kizza, Paul Willa, Khalid Lwaliwa, John Revita, Joackim Ojera, Ben Ocen, Shafik Kagimu, Allan Okello, Fahad Bayo na Bright Anukani

Chanzo: mwananchi.co.tz