Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uganda leo wanapiga kura

66d202794bbd758d037e67170995b3dc.png Uganda leo wanapiga kura

Thu, 14 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WANANCHI wa Uganda leo wanapiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa rais, wabunge na madiwani huku mchuano mkali ukitarajiwa kuwa kati ya mgombea wa chama tawala cha NRM ambaye ni Rais, Yoweri Museveni (pichani) na mgombea wa upinzani kupitia vuguvugu la ‘Nguvu ya Umma’.

Kampeni za uchaguzi huo ambazo zilifungwa juzi hazikuwa na shamrashamra kama zilivyokuwa kampeni za chaguzi zilizopita kwa sababu ya kuwepo kwa sheria kali za kuzuia kusambaa kwa Virusi vya Corona.

Kutokana na hofu ya kutokea kwa vurugu katika uchaguzi huu, jana serikali ilifunga kwa muda mitandao ya kijamii ambayo imeonekana kutumiwa na watu wasiokuwa na nia njema na uchaguzi huo kuleta uchochezi.

Hatua hiyo imeshutumiwa vikali na jumuiya ya kimataifa wakisema ni ukandamizaji wa haki za binadamu na kunyima wapinzani haki ya msingi ya kuwasiliana na wananchi.

Mwanadiplomasia mkuu wa Marekani barani Afrika, Tibor Nagy pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, wameelezea wasiwasi wao kuhusu hatua hiyo na kuitaka Uganda kuheshimu haki za binadamu kuelekea uchaguzi huo.

Mbali na hao, Balozi wa Marekani nchini Uganda ameeleza kusikitishwa na hatua ya serikali ya kukataa kuwapatia wasimamizi wao idhini ya kusimamia uchaguzi.

Balozi Natalie Brown amesema kuwa zaidi ya asilimia 75 ya maombi ya idhini za ujumbe wa wakaguzi wa Marekani yalikataliwa.

Akijibu shutuma kutoka kwa jumuiya ya kimataifa, Rais Yoweri Museveni alisema serikali yake imefungia mitandao ya kijamii nchini humo kuelekea uchaguzi wa rais akisema mitandao hiyo imekuwa jeuri baada ya mitandao hiyo kufunga akaunti kadhaa zinazohusishwa na kampeni yake kutaka achaguliwe tena.

Katika hotuba yake aliyoitoa juzi usiku Rais Museveni alisema ana uhakika serikali imefunga mitandao ya kijamii kwa maslahi ya wananchi wa Uganda na amewaomba msamaha Waganda kwa hali hiyo.

Chanzo: habarileo.co.tz