Wizara ya Afya nchini Uganda imesema kuwa wasafiri wote watakaoingia nchini humo watatakiwa kulipa dola 30 sawa na Tsh 70,000 kwa ajili ya malipo ya kipimo cha Corona ambacho ni lazima kufanyika.
Wizara hiyo imeielekeza Mamlaka ya usafiri wa anga kusimamia agizo hilo kwa kila ndege itakayoshusha abiria wake katika taifa hilo linalopambana kudhibiti wimbi la tatu la Corona.
Agizo hilo linakuja kuondoa utaratibu wa awali uliowekwa wa kupima abiria wanaowasili kutoka katika mataifa yaliyoshambuliwa zaidi na ugonjwa huo.
"Mpago huu umelenga katika kudhibiti kasi ya maambukizi ya Corona nchini, kupambana na viashiria vyote vya wimbi la tatu la ugonjwa huu" Imesema taarifa ya Mamlaka ya Anga Uganda.
Wizara hiyo imesema kuwa tayari imeshaandaa maabara maalumu kwenye viwanja vyote vya ndege kwa ajili ya kukamilisha zoezi hilo.