RAIS Yoweri Museveni amezindua rasmi kliniki ya kwanza ya majaribio ya dawa za asili za ugonjwa wa covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona.
Majaribio ya dawa za corona yatakayofanywa katika kliniki hiyo iliyopo Hospitali ya Mulago ni zile zinazozalishwa nyumbani ambazo zimeendelezwa na wanasayansi wa nchini kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Chuo Kikuu cha Makerere Shule ya Afya, Hospitali ya Mulago na wadau wengine.
Rais Museveni amewapongeza wanasayansi waliohusika katika kufanya utafiti wa dawa hizo na kuahidi kutoa kipaumbele kwa sekta hiyo.
“Nawapongeza wanasayansi wa Uganda kwa kuja na tiba ya covid-19 ambayo imeleta tabasamu kwa wagonjwa nchini,” alisema Museveni na kuongeza kwa sasa wapo katika jitihada za kupata chanjo ya cotona ili kuweza kujikinga na ugonjwa huo.
Waziri wa Afya, Jane Ruth Aceng alisema dawa hizo zimeshapitia uhakiki mbalimbali na kupata vyeti muhimu na kuthibitishwa na Mamlaka ya Dawa ya Taifa, Shirika la Viwango Uganda na Baraza la Sayansi na Teknolojia kuwa ni salama kutumiwa na binadamu.