Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uganda iko kwenye tahadhari wanamgambo wa ADF kuvuka mpaka kutoka DR Congo

Uganda Iko Kwenye Tahadhari Wanamgambo Wa ADF Kuvuka Mpaka Kutoka DR Congo Uganda iko kwenye tahadhari wanamgambo wa ADF kuvuka mpaka kutoka DR Congo

Tue, 19 Mar 2024 Chanzo: Bbc

Vikosi vya usalama vya Uganda viko katika hali ya tahadhari baada ya kusema wapiganaji wa kundi lenye mafungamano na Islamic State waliingia nchini humo mwishoni mwa juma.

Wanamgambo wa Allied Democratic Forces (ADF) wanapanga mashambulizi katika maeneo ya mijini, maeneo ya ibada, shule na matukio ya umma, kulingana na jeshi.

Iliwataka wananchi kuwa waangalifu "ili kuepuka kuwa waathirika wa ugaidi wa ADF".

ADF imehusishwa na mfululizo wa mashambulizi mabaya nchini Uganda, ikiwa ni pamoja na kulenga shule mwezi Juni mwaka jana.

Asili ya kundi hilo ni nchini Uganda katika miaka ya 1990 na watu waliochukizwa na jinsi serikali inavyowatendea Waislamu.

Lakini baada ya kusambaratishwa na jeshi, mabaki hayo yalitorokea mpakani hadi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Mnamo 2021, Uganda na DR Congo zilianzisha mashambulizi ya pamoja kuwafukuza ADF kutoka ngome zao za Kongo, lakini hadi sasa zimeshindwa kukomesha mashambulizi ya kundi hilo.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema mara kadhaa operesheni hiyo imefanikiwa kuua idadi kubwa ya wapiganaji wa ADF wakiwemo baadhi ya makamanda.

Lakini ADF imeshutumiwa kwa kuendelea kufanya mashambulizi ikiwa ni pamoja na katika shule moja magharibi mwa Uganda mwezi Juni mwaka jana, wakati makumi ya wanafunzi waliuawa.

Mnamo Oktoba mwaka jana, kundi hilo hilo lililaumiwa baada ya wanandoa waliokuwa wakifunga ndoa na muongoza watalii kutoka Uganda kupigwa risasi na kufariki katika mbuga ya wanyama.

Naibu msemaji wa jeshi la Uganda Kanali Deo Akiiki alisema katika taarifa iliyotolewa Jumatatu kwamba kundi la wanamgambo wa ADF lilivuka Uganda kutoka DR Congo siku ya Jumamosi.

"Kundi hili linashukiwa kuwa chini ya amri ya kamanda maarufu wa ADF Ahamed Muhamood Hassan, almaarufu Abu Waqas, mtaalamu wa mabomu wa ADF mzaliwa wa Tanzania," iliongeza taarifa hiyo.

Jeshi hilo liliwataka wananchi kubaini na kutoa taarifa kwa watu wanaotilia shaka.

Chanzo: Bbc