Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ugaidi watajwa kuongezeka zaidi Afrika

Ugaidii Kuongezeka.png Ugaidi watajwa kuongezeka zaidi Afrika

Thu, 25 Aug 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kuenea kwa hujuma za kigaidi katika kanda tofauti za bara Afrika, hasa kuongezeka kwa mashambulizi yanayotekelezwa na makundi ya Al-Shabaab huko Somalia na Boko Haram nchini Nigeria, kumepelekea kuibuka wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa ukosefu wa usalama barani Afrika na duniani kote.

Kuhusiana na suala hilo, Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia amesisitiza utayarifu wa nchi hiyo kwa ajili ya kupambana na kundi la kigaidi la al-Shabaab na kusema: "Serikali ya shirikisho ya Somalia imeazimia kuwaangamiza magaidi wa Al-Shabaab kijeshi , kiuchumi na kiitikadi."

Kauli ya rais wa Somalia imekuja siku chache baada ya kundi hilo la kigaidi kushambulia Hoteli ya Hayat mjini Mogadishu na kupelekea watu zaidi ya 21 kupoteza maisha.

Ijapokuwa nchi za Kiafrika zinakabiliwa na changamoto nyingi katika nyanja mbalimbali za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiusalama, lakini uwepo wa makundi ya kigaidi katika bara hilo na hofu ya kupanuka shughuli zao katika nchi tofauti hivi sasa imekuwa moja ya kero kuu.

Kuwepo kwa kundi la kigaidi la Boko Haram katika eneo la Magharibi mwa Afrika hususan Nigeria na nchi jirani pamoja na harakati za kundi la Al-Shabaab katika eneo la mashariki mwa Afrika hususan Somalia na nchi za mpakani kumevuruga usalama katika bara la Afrika. Kushindwa kwa kundi la kigaidi la ISIS au Daesh katika eneo la Asia Magharibi na ukosefu wa utulivu wa kisiasa sambamba na kutokuwepo kwa serikali kuu yenye nguvu nchini Libya kumesababisha kundi hilo la kigaidi kuzidisha shughuli zake barani Afrika.

Ijapokuwa nchi za Kiafrika zimechukua hatua za kupambana na ugaidi katika miaka ya hivi karibuni, mivutano ya kisiasa, ukosefu wa fedha na utegemezi wa kigeni wa baadhi ya serikali za Afrika umesababisha shughuli za makundi ya kigaidi kuongezeka hasa katika miezi ya hivi karibuni katika maeneo mbalimbali ya bara hilo. Makadirio yanaonyesha kuwa kuanzia Januari hadi Juni 2022, kundi la kigaidi la ISIS lilifanya mashambulizi 305 Afrika Magharibi.

"Nikolai Patrushev," katibu wa Baraza la Usalama la Russia amesema kuhusiana na suala hilo: "Kwa kusambaratika makundi ya kigaidi ya kimataifa huko Iraq na Syria, sasa makundi hayo yanapanua shughuli zao katika nchi za Asia Kusini na bara la Afrika."

Katika miezi ya hivi karibuni, mgogoro wa Ukraine pia umesababisha ongezeko la wasiwasi wa upatikanaji chakula na kutokana na kupungua kwa uwekezaji wa kigeni, umaskini na mfumuko wa bei umeongezeka katika nchi nyingi za Afrika. Kwa upande mwingine, hatua kali zilizochukuliwa na nchi za Ulaya katika mipaka ili kuzuia wahamiaji, zimepelekea kupungua idadi ya wahamiaji wanaoingia Ulaya. Suala hilo limesababisha vijana wengi kujiunga na vikundi vya kigaidi kutokana na kukosekana fursa za ajira.

"Jacob Mandy", mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Colgate cha New York, anasema kuhusu suala hili kuwa: "Sababu kuu ya kuenea makundi ya kigaidi ni umaskini uliokithiri. Hata kama serikali zinakidhi mahitaji ya wananchi, uwezo wao katika maeneo mengi ni mdogo na katika baadhi ya maeneo haupo kabisa. Vijana wengi sasa wanaona kujiunga na vuguvugu kunaweza kuibua fursa katika maisha yao."

Kwa upande mwingine hakuna azma ya dhati ya kukabiliana na makundi ya kigaidi miongoni mwa baadhi ya viongozi wa nchi za Kiafrika. Serikali nyingi za Kiafrika hazina uwezo au azma imara ya kutokomeza makundi ya kigaidi. Kwa upande mwingine, hata baadhi ya nchi za Magharibi zinaunga mkono makundi ya kigaidi nyuma ya pazia, kwa sababu ongezeko la ukosefu wa usalama linaweza kuhalalisha uwepo wao wa kisiasa na kijeshi katika bara hilo.

Hivyo ingawa rais wa Somalia ameahidi mapambano makali dhidi ya magaidi wa al-Shabaab, lakini ni wazi kuwa nchi hiyo haina uwezo wa kufanikiwa katika uwanja huo bila kuwepo msaada wa kimataifa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live