Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ufaransa yatoa bil 84/- kuunganisha umeme Tanzania, Zambia

E7dd0b022e6922d2dc7697ca05c96445 Ufaransa yatoa bil 84/- kuunganisha umeme Tanzania, Zambia

Wed, 16 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

SERIKALI ya Tanzania imesaini mkataba wa Sh bilioni 84 (Euro milioni 26) na Umoja wa Ulaya kupitia Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) kwa ajili ya kugharamia mradi wa kuunganisha umeme Tanzania na Zambia.

Mkataba huo ulisainiwa jana jijini Dar es Salaam kati ya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James na Balozi wa Ufaransa hapa nchini, Frederick Calvier.

James alisema katika mradi huo, Tanzania inaishia mpakani na Zambia wataunganisha kuanzia hapo kwenda nchini mwao umeme wa msongo Kv 400 ili Tanzania inapokuwa na umeme wa ziada iweze kuwauzia nchi jirani na wao kama watakuwa na umeme wa ziada wataweza kuiuzia Tanzania.

“Kiasi cha fedha tulichopewa leo(jana) na Umoja wa Ulaya kupitia Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) ambao ndiyo wasimamizi wa fedha hizi ambazo ni msaada na siyo mkopo zitaenda kujazilia sehemu ile ya gharama kubwa ya kujenga njia ya kusafirishia umeme kutoka Iringa-Mbeya-Sumbawanga jirani na nchi ya Zambia,”alisema James.

Alisema Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 ililenga kufikia uchumi wa kipato cha kati cha chini ambacho tayari kimefikiwa na taifa linajitahidi kufikia uchumi wa kipato cha kati cha juu.

Alisema gharama za jumla za mradi huo ni Dola za Marekani milioni 591 ambazo sawa na Sh trilioni 1.35 kutoka kwa wafadhili mbalimbali.

Miongoni mwa fedha hizo Sh trilioni 1.35 zimo Sh bilioni 84 zilizotolewa jana na EU, Euro milioni 100 za mkopo wa masharti nafuu kutoka AFD na zingine mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia (WB) Dola za Marekani milioni 455 ambazo zinafikia jumla ya Dola milioni 591.

“Msaada huu unaonesha kwamba Serikali ya Ufaransa na Umoja wa Ulaya ni marafiki wazuri wa Tanzania kinyume na dhana ambayo imejengeka ya kuwa uhusiano wetu umekuwa wa wasiwasi, kwa hiyo naomba wale ambao wanadhani nchi yetu haiko sawa na wadau wa maendeleo, kitendo hiki leo(jana) kinawatoa kabisa kwenye mstari na wanabakia na aibu,” alisema James.

Naye Balozi Clavier alisema nchi yake inaunga mkono malengo ya kimaendeleo ya Tanzania na jitihada za Rais John Magufuli za kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati kwa faida ya watu wa Tanzania.

Clavier alisema umeme ni muhimu kwa kuwa unasaidia kukua kwa shughuli za kiuchumi na kusainiwa kwa mkataba huo ni alama ya ushirikiano mzuri uliopo kati ya Umoja wa Ulaya, AFD, Ufaransa na Tanzania.

Mwakilishi wa AFD hapa nchini, Stephanie Essombe, alisema amefurahishwa na hatua ya kusainiwa kwa mkataba huo ambao utasaidia kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika hapa nchini.

Kwa upande wake Mwakilishi wa EU hapa nchini, Cedric Merei alisema upatikanaji wa umeme wa uhakika unaenda sambamba na upatikanaji wa huduma bora za jamii.

Naye Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati, Edward Ishengoma, alisema kusainiwa kwa mkataba huo ni muhimu kwa Tanzania kwa sababu utahakikisha kuwepo kwa nishati ya uhakika na ya kutosha na utasambazwa kwa wananchi, kusafirisha umeme wa ziada kwa nchi jirani kutokana na kuwepo kwa mfumo wa kusafirisha umeme katika nchi zinazoshirikiana kwa ukanda wa Afrika Mashariki na nchi za Kusini mwa Afrika.

Chanzo: habarileo.co.tz