Dar es Salaam. Tofauti na makadirio ya kukua kwa asilimia 2.4 mwaka 2019, Benki ya Dunia (WB) imesema uchumi wa Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara unatarajia kusinyaa kwa kati ya asilimia 2.1 na asilimia 5.1 mwaka huu.
Ripoti ya tathmini ya mwenendo wa uchumi ijulikanayo kama Africa’s Pulse inayotolewa mara mbili kila mwaka inaonyesha uchumi utayumba kutokana na athari za kuenea kwa virusi vya corona.
Mwenendo huo ni tofauti na matarajio yaliyokuwapo awali kabla ya mlipuko wa corona benki hiyo ilipotabiri uchumi ungekua kwa asiliia 3.9 mwaka 2020.
Wakati uchumi wa Tanzania ukitabiriwa kukua kwa zaidi ya asilimia sita mwaka huu, huenda hilo lisifanikiwe kutokana na mlipuko wa virusi vya corona vilivyotikisa uchumi wa dunia.
Taarifa iliyotolewa leo, Aprili 9, 2020 na mchumi mkuu wa benki hiyo kwa Afrika, Albert Zeufack jijini Washington inasema kutokana na kusambaa kwa ugonjwa huo, bara hili litapoteza kati ya Dola 37 bilioni hadi Dola 79 bilioni za Marekani kutokana na kusimama kwa biashara, uwekezaji na ufadhili kutoka kwa wahisani.
“Mataifa mbalimbali yanachukua hatua za kisera kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa wa corona. Benki kuu zinapunguza riba na kuzisaidia benki za biashara kuwa na ukwasi wa kutosha. Ni muhimu kukumbuka usalama wa jamii hasa wafanyakazi wa sekta isiyo rasmi katika ujenzi wa uchumi hapo baadaye,” amesema Zeufack.
Pia Soma
- Polisi yapiga marufuku mikusanyiko ya ufukweni, baa jijini Dar sikukuku ya pasaka
- Sakata la mameya wa Chadema kuondolewa madarakani latinga bungeni
- VIDEO: Waziri Ummy asema maambukizi ya corona sasa ni ya ndani
Makamu wa rais wa benki hiyokwa Afrika, Hafez Ghanem anasema kusitishwa kwa biashara baina ya mataifa kumeathiri uchumi wa dunia kwa kiasi kikubwa hivyo hatua za haraka zinahitaji kuchukuliwa.
“Tunajitahidi kutumia rasilimali zilizopo kuzisaidia Serikali kulinda watu wao pamoja na ajira kwa kuomba kusitishwa kwa ulipaji wa madeni ili fedha hizo zitumike kuihudumia jamii na kuinu abiashara za wajasiriamali wadogo na wa kati,” amesema Ghanem.
Ingawa ugonjwa huo unaziathiri nchi nyingi duniani, rais huyo amesema Afrika itaathirika zaidi kutokana na uzalishaji mdogo wa huduma na bidhaa kwa kuzingatia kuwa hutegemea kuagiza nyingi kutoka nje pamoja na kuathirika kwa sekta ya utalii lililochangiwa na kuzuiwa kwa safari za kimataifa.
"Watunga sera Afrika wajikite kuokoa maisha ya watu, kuboresha huduma za afya na kuhakikisha hakuna ukosefu wa chakula wakati huu," amesema Ghanem.
Mabadiliko haya y amwenendo wa uchumi yataihusu Tanzania pia kwa viwango tofauti na mataifa mengine. Ingawa Serikali inaamini uchumi utakua kwa asilimia 7, benki hiyo ilikadiria ungekua kwa asilimia 5.8 mwaka huu huku Shirika la Fedha Duniani (IMF) likisema utakua kwa asilimia 6.