Uchumi wa Afrika Kusini umeshuka kwa asilimia 0.2 katika robo ya tatu ya mwaka kufuatia miezi sita ya ukuaji wa taratibu na kusababisha matatizo kwa Serikali.
Hayo yanajiri wakati nchi hiyo ikielekea kwenye uchaguzi utakaofanyika mwakani.
Sekta za kilimo, viwanda na ujenzi zimekuwa na mchango kwenye Pato la Taifa katika nchi hiyo iliyoendelea zaidi katika viwanda barani Afrika kuanzia Julai hadi Septemba.
Shirika la Habari la AFP katika taarifa yake lilieleza hayo ni kwa mujibu wa Wakala wa Taifa wa Takwimu (StatsSA).
Afrika Kusini inaelekea kwenye uchaguzi mkuu mwaka 2024 kukiwa na ukosefu mkubwa wa ajira katika uchumi ambao umekuwa ukidorora kwa miaka kadhaa.
Mdororo wa hivi karibuni unafuatia kusuasua kwa ukuaji wa la Pato la Taifa kwa asilimia 0.4 na asilimia 0.5 katika robo mbili za kwanza na ya pili.
Kwa muda Afrika Kusini imekumbwa na tatizo la muda mrefu la nishati ya umeme ambao umekuwa ukikatika hadi saa 12 kwa siku.
Matatizo katika kampuni za reli na bandari ya umma kumekuwa na kuibuka kwa kashfa za ufisadi, wizi huku matengenezo, yakitatiza zaidi shughuli za kiuchumi.
StatsSA imesema sekta ya kilimo ilishuka kwa kasi zaidi katika robo ya tatu na ambapo mchango wake katika pato la taifa ulipungua kwa asilimia 9.6.
Sekta hiyo ilikabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwamo mlipuko wa mafua ya ndege na mafuriko katika jimbo la Kusini la Western Cape.
Mahitaji kidogo ya bidhaa mbalimbali yalisababisha uzalishaji wa viwanda kupungua kwa asilimia 1.3 wakati uzalishaji wa madini ukirudi nyuma kwa asilimia 1.1.
Chama kikuu cha upinzani nchini humo, Democratic Alliance kilitoa maoni juu ya takwimu za hivi karibuni za pato la taifa kikisema ni matokeo ya sera zilizopo.