Ghadhabu zilipanda katika kituo cha kitaifa cha kuhesabia kura cha Bomas of Kenya usiku wa Alhamisi wakati tume ya uchaguzi ilipoanza kuhakiki matokeo ya uchaguzi wa urais.
Maafisa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) walitatizika kudumisha utulivu baada ya Chama cha United Democratic Alliance (UDA) kudai kuwa fomu 34A ambazo hazijaidhinishwa zilikuwa zikiingizwa kinyemela katika ukumbi huo.
Mawakala wa mgombea urais William Ruto walizozana na maafisa wa uchaguzi kuhusu fomu zinazotiliwa shaka, na kuzua taharuki ambayo ilifanya makamishna wa IEBC kuingilia kati. Katibu Mkuu wa UDA, Veronica Maina, walitishia kujiondoa katika mchakato wa kupokea na kukusanya fomu 34A na 34B.
Bi Maina aliwashirikisha maafisa wa bodi ya kura kwenye dawati la kuhakiki ubora kabla ya mawakala wengine wa UDA kujiunga nao kwa dakika 10.
Mawakala wa UDA pia walikuwa wamelalamikia idadi ya watu walioruhusiwa kwenye madawati manne yaliyowekwa kwa ajili ya uhakiki na uchukuaji fomu.
Mkuu wa masuala ya ushirika wa IEBC Tabitha Mutemi baadaye aliamuru maajenti ambao hawakuidhinishwa katika ukumbi huo kuondoka.
Huku hayo yakijiri tume ya IEBC imesema kuwa wameanzisha mchakato wa uhakiki wa ngazi nne, kuashiria kuwa huenda tangazo la matokeo ya mwisho likafanywa wikendi.
Kamishena wa tume hiyo Prof Abdi Guliye alisema tume imeunda madawati manne kwa ajili ya uhakiki wa matokeo kutoka katika majimbo 291 ya uchaguzi yakiwemo magereza na kure zilizopigwa nje ya nchi.