Mkurugenzi Mtendaji wa SportPesa, Ronald Karauri ameshinda kinyang'anyiro cha Ubunge katika jimbo la Kasarani kwa tiketi ya Kujitegemea.
Karauri alipata kura 32,406. Mpinzani wake wa karibu John Kamau (UDA) alipata kura 30,444 huku Mercy Gakuya (Jubilee) akipata kura 24,790.
Jumla ya waliojiandikisha kupiga kura katika eneo la Kasarani walikuwa 155,405, huku waliojitokeza kupiga kura wakiwa 91,774.
Akipokea cheti chake kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi Nyongesa Chelai, mbunge huyo mteule alisema wananchi wameachana na mawazo ya kuchagua vyama vya siasa badala yake wamechagua chaguo lao.
"Ninataka kuwashukuru watu wa Kasarani kwa kunichagua," Karauri alisema.