Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uchaguzi wa Uganda na somo kwa wanasiasa wa Afrika

387d5441b7b2279aef57bd33a8a73f33 Uchaguzi wa Uganda na somo kwa wanasiasa wa Afrika

Wed, 20 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

TUME ya Uchaguzi ya Uganda mnamo Februari 16, mwaka huu ilitangaza matokeo ya uchaguzi yaliompa ushindi Yoweri Kaguta Museveni kwa kupata kura 5,851,037 sawa na asilimia 58.64 huku mpinzani wake wa karibu Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine akipata kura 3,475,298 sawa na asilimia 34.83.

Kwa matokeo hayo Rais mteule wa Uganda ni Yoweri Museveni.

Kama ilivyo kawaida ya watu wanaoshindwa Kyagulanyi alijitokeza kabla hata ya tume kumaliza kutangaza matokeo akidai kuibiwa kura na kwamba matokeo ni batili sawa na alivyofanya rais wa Marekani, Donald Trump na aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nchini, Tundu Lissu.

Kwa mujibu wa Kyagulanyi, Uchaguzi wa Uganda ulisheheni wizi wa kura ambao haujapata kutokea katika historia ya Uganda! Sasa swali nililojiuliza, ni muda gani amefanya utafiti na kugundua kuna wizi wa kura kiasi ambacho haijawahi kutokea? Nauliza haya kwasababu hata Trump aling’ang’ania hoja hii pasipo mafanikio.

Hadi leo anadai uchaguzi uliomfanya Joe Biden awe Rais wa Marekani ulijaa wizi uliokithiri japo kila alitaka kura zihesabiwe upya, matokeo yalionesha ameshindwa. Yaliofanyika Marekani ndio sasa na Kyagulanyi anayafanya.

Kwa upande wa Tanzania, sote tunakumbuka Lissu alidai uchaguzi ulijaa wizi kisha kutaka watu waingie mtaani kupinga matokeo hayo yaliompa ushindi wa kishindo Rais John Magufuli lakini baada ya raia kugoma, yeye akaondoka nchini.

Hali hii ni sawa na alichofanya Kyagulanyi ambaye alitorosha familia yake kwanza hata kabla ya uchaguzi akidai ni kwa usalama wake.

Mara baada ya Tume ya Uchaguzi kutangaza matokeo Museveni alihutubia wananchi na kugusia mambo makuu ya msingi yatakayokuwa vipaumbele vya chama chake katika kipindi hiki cha uongozi.

Baadhi ya mambo hayo ni pamoja na elimu bure, kuzuia mianya ya rushwa kwa kila idara, kusimamia misingi ya Uganda mpya, kudumisha uzalendo, kuzuia mianya ya kuingiliwa katika siasa na maamuzi yanayohusu Uganda kutoka mataifa ya nje hasa ya magharibi.

Pia alizungumzia kutolipisha kodi wafanyabiashara ndogondogo, kuacha kutumikia matumbo na kutoruhusu bajeti inayolenga kufaidisha wachache hasa wabunge. Katika ngwe hii ya utawala ameahidi kuwa mkali sana kwa maslahi mapana ya Uganda.

Pamoja na mambo mengine Museveni alitumia muda mwingi kufundisha vijana wanaoingia kwenye siasa kuwa na malengo ya kusaidia nchi zao hasa nchi za Afrika kuliko kutanguliza maslahi ya mataifa ya ulaya na Amerika.

Museveni alisisitiza kwamba wanasiasa wengi hasa wa vyama vya upinzani Barani Afrika, wanaingia katika siasa pasipo kuwa na malengo wala maono ya nchi. Alisema, “Ni hatari sana kuingia kwenye siasa kama hujui nini unataka au kama huna maono ya nchi”

Hoja hii ya Museveni ina mashiko mapana sana hasa kwa wanasiasa wetu wa vyama vya upinzani ambao mara nyingi wameonekana kutokuwa na ajenda za msingi badala yake hutumia muda wa kampeni kutukana na kukosoa watu badala ya kuwa na sera na kuzinadi.

Jambo hili huwafanya wanasiasa hawa kuonekana ni vibaraka wa mataifa ya kigeni na kimsingi uwezeshaji wao mkubwa huitegemea kutoka huko. Na kwa kuwa wanawategemea sana basi hutumia hata vyombo vyao vya habari kufikisha jumbe zao huku wakikubali kutumika kuzichafua nchi zao.

Ukweli kuna haja ya wanasiasa wetu kujiangalia na kujitathmini upya. Jambo la msingi katika siasa ni sera siyo kueneza chuki na kuhakikisha waliopewa dhamana ya kuongoza, wanatatua kero za wananchi.

Mfano mara nyingi tumeshuhudia katika maeneo mengi akipita Rais ndio wananchi wanaeleza kero zao ambazo kimsingi zilipaswa kushughulikiwa na viongozi waliopo katika eneo husika. Badala yake viongozi hawa kazi yao huwa ni kulalamikia serikali badala ya kueleza changamoto za wananchi ili zishughulikiwe.

Pamoja na mambo mengine hotuba ya Rais Museveni ilinifurahisha katika eneo la kutoruhusu kuingiliwa na mataifa ya nje hasa ya Ulaya na Amerika katika siasa za Uganda.

Kwa mujibu wa Museveni mataifa haya mara nyingi hutumia udhaifu uliopo kusababisha ghasia ndani ya mataifa ya Afrika. Na kimsingi mataifa haya huwa na lengo moja tu la kuiba rasilimali zilizopo kwenye eneo husika. Na kila inapohitajika hutumia wanasiasa wa nchi husika wenye kupigania matumbo yao wenyewe kueneza ghasia.

Ajenda ya kutoruhusu kuingiliwa katika mambo ya Uganda ni jambo la msingi ambalo linapaswa kuigwa na mataifa mengi ya Afrika. Kuruhusu kuingiliwa na mataifa ya kigeni kumeharibu taifa la Libya, Afrika Kusini na mataifa mengine ambayo yanapata misukosuko sababu ya muingiliano huu.

Afrika inahitaji kuungana na kupambana na ukoloni mamboleo ambao unaletwa na mataifa makubwa kwa hoja ya demokrasia. Nchi kama Ujerumani, Angela Marcel ametawala miaka 16, Uingereza hadi sasa Queen Elizabeth anaongoza kana kwamba Mungu aliumba familia yake tu ndo iongoze Uingereza, na mataifa mengineyo yenye mifano hiyo.

Natambua katika kipengele hiki msomaji unaweza usinielewe lakini ukweli ni kwamba watu hawali demokrasia, hula mkate. Kinachohitajika ni kiongozi mwenye maono ya kuunganisha wananchi wake likiwa jambo la kwanza na kisha kuwatengenezea mazingira ya kupambana na umasikini. Si kuhubiri nani kakaa muda mrefu madarakani.

Kama Waganda wamemchagua Rais Museveni, taifa jingine lisiwaingilie, hiyo ndiyo demokrasia yao. Kwanza si desturi yetu kama Waafrika kuingilia masuala ya familia ya jirani.

Bara la Afrika limezidi kubaki nyuma kimaendeleo kwasababu ya mataifa haya makubwa kuingilia mambo yake. Migogoro inaoendelea Afrika ni kwasababu hiyo. Mbona sisi hatuendi kuingilia mambo yao? Ya nini wao waingilie yetu?

Jibu ni moja tu, wanataka kuendelea kututawala na kuiba rasilimali zetu. Kama Waafrika tuzinduke na kuanzisha tena wimbo wa uhuru wa kifikra na muungano wa Afrika yote.

Rais Museveni alichokoza ajenda za msingi katika hotuba yake, mfano alihoji mbona hajasikia hata siku moja wanasiasa wetu hasa wa upinzani wakizungumzia juu ya Muungano wa Afrika? Aliongeza kwamba Afrika imekuwa kama Latin Amerika, yaani eneo lisilo na maono?

Kama wazungu wanataka kuingilia mambo ya Afrika basi wajikite kwenye kuhamasisha muungano wa Afrika. Lakini hawawezi kufanya hivyo kwasababu Afrika ikiungana dunia nzima itakosa sehemu ya kuiba, itakosa masoko badala yake Afrika ndo litakuwa taifa tajiri na kubwa kuliko yote ulimwenguni; ki uhalisia hawako tayari kuona hilo likitokea.

Badala yake wanaishia kuhubiri viongozi kukaa madarakani muda mrefu! Matumizi mabaya ya rasilimali zetu kana kwamba wao ndiyo waliotupatia hizo rasilimali! Mambo haya kimsingi yanaidhoofisha Afrika.

Hatuwezi kuwa na wanasiasa ambao kazi yao kubwa ni kusikiliza wazungu wanasemaje juu yao. Tunakuwa kama watoto wanaosubiri kusikia wazazi wao wanasema nini juu yao. Hii siyo sawa.

Tunapohubiri uzalendo tugusie muungano wa Afrika, hii ndiyo njia pekee ya kuiondoa Afrika chini ya ukoloni mambo leo. Na kuenzi ndoto za wazee wetu akiwamo Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa zamani wa Ghana, Kwame Nkrumah na wengine.

Nchi kama Tanzania inaweza kuwa shahidi kwa haya aliyosema Rais Museveni. Wakati Dk John Magufuli akijitahidi kuiondoa Tanzania katika dimbwi la umaskini wanasiasa wetu uchwara walimbeza na wanaendelea kufanya hivyo kisa tu mataifa ya magharibi na mashariki yanasema hivyo! Huu ni ukosefu wa uzalendo.

Hakuna taifa kubwa linaloweza kufurahia wakati mnyonge wake anahangaika kujikwamua. Lazima wataendelea kumkwamisha ili asifikie malengo. Mapenzi mema kwa nchi na Afrika kwa ujumla ndiyo yanayomfanya Rais Magufuli aendelee kulijenga taifa letu.

Wakati anazuia wizi wa madini wengine walidiriki kusema kwamba tutashtakiwa kama taifa na tutashindwa. Hata hivyo ni msimamo pekee wa Dk Magufuli uliotusaidia Watanzania ikiwamo kushughulikia mambo ya ndani wenyewe badala ya kutegemea mataifa ya nje na hii imewezesha Tanzania kufikia katika nchi ya uchumi wa kati Julai 2019 ilipotangazwa na Benki ya Dunia.

Kwa Rais Museveni, uzalendo unahusisha mapenzi dhidi ya Afrika, Afrika Mashariki na Uganda. Hatoruhusu kiongozi yeyote ambaye analenga kuhubiri ukabila ndani ya taifa hilo. Kimsingi, sijui wanasiasa wetu wa upinzani huwa wana mdudu gani vichwani, mara nyingi hupenda kuhubiri siasa za kuwatenga wananchi aidha kwa ukabila au kwa ukanda au udini.

Hii ni makosa makubwa kwa mustakabali wa taifa lolote duniani. Lakini kwa kuwa wao hulenga matumbo yao wenyewe hutumia vigezo hivyo vya kuwagawa wananchi ili wapitie humo kupata ushindi. Uzuri kuwa wanashindwa wakati wote.

Akizungumza kuhusu kufungia mitandao ya kijamii, Musemevi anasema ilikuwa na lengo la kupunguza mataifa ya ulaya na Amerika kuingilia siasa za Uganda hasa wakati huo nyeti wa uchaguzi. Na kimsingi hii inaleta mantiki.

Mara nyingi mataifa haya yamekuwa yanatumia mitandao ya kijamii kuleta machafuko kwenye mataifa ya Afrika. Kama wanaopiga kura ni wananchi na mara nyingi wapiga kura wengi hasa wa vijijini ambao wengi ndio wapiga kura hawatumii mitandao ya kijamii kwa sababu ya mazingira na wagombea huenda kujinadi kwao, kuna haja gani ya mitandao ya kijamii ambayo mingi hutumika kupotosha umma kwa taarifa za uongo na kuvuruga amani?

Kwa namna moja au nyingine hotuba ya Rais Museveni inalenga kuwaamsha wanasiasa wa Afrika kuacha kuabudu mataifa mengine badala yake kubeba mapenzi mema ya nchi zao na kupigania uhuru halisi wa mataifa husika dhidi ya ukoloni mambo leo na kujikwamua kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Mwandishi wa Makala haya ni mchangiaji wa gazeti hili. Mawasiliano yake ni +255 712 246001; [email protected]

Chanzo: habarileo.co.tz