Serikali ya Kenya imejitenga na matamshi yaliyotolewa kwenye kikao cha waandishi wa habari mjini Nairobi na wanasiasa kadhaa wa Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo (DRC) na makundi kadhaa yakiwemo kundi la waasi wa M23, kuwa wameunda vuguvugu jipya kwa jina la Muungano wa Mto Congo au Congo River Alliance.
Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Jumapili Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Musalia Mudavadi, amesema kuwa serikali ya Kenya haikuhusika au haikujulishwa kuhusiana na kikao hicho kilichofanyika siku ya Ijumaa katika mji Mkuu wa Nairobi.
Hata hivyo Mudavadi amesema kuwa kikao hicho na wanahabari kilifanyika jijini humo kwa misingi kuwa nchi ya Kenya inaruhusu uhuru wa kujieleza kwa raia wake na raia wakigeni.
Mudavadi ameongeza kuwa serikali ya Kenya inachunguza madai kuwa wanasiasa hao walitoa matamshi kuwa wana mahusiano na makundi ya waasi nchini DRC na pia matamshi ambayo yanaweza kuwa kinyume cha sheria ya DRC.
Amesema kuwa serikali imeanzisha uchunguzi kubainisha ikiwa matamshi hayo yalidhamiria kuvuruga utawala wa kikatiba nchini Congo.
Tamko hili la serikali ya Kenya limejiri baada ya serikali ya DRC hapo jana kumtaka Balozi wa Kenya jijini Kinshasa kuwapa maelezo ya kile kilichotokea jijini Nairobi.
Serikali ya DRC pia imeamua kumrejesha nyumbani balozi wake nchini Kenya ili kufanya mazungumzo nae. Aidha DRC pia imemuagiza balozi wake katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ambaye pia ni balozi wake nchini Tanzania kurejea nyumbani kwa mazungumzo.
Mmoja kati ya waliozungumza katika mkutano wa Nairobi ni aliyekuwa rais wa tume ya Uchaguzi nchini DRC, CENI Cornel Naanga, ambaye sasa ni miongoni mwa wanaopinga utawala wa rais Felix Tsishekedi, na adai kuwa uchaguzi unaopangwa kufanyika wiki ijayo hautakuwa wa huru na haki.
Duru za kisiasa zinaonesha kuwa mkutano huo wa Nairobi umehujumu mahusiano ya Kenya na DRC, na hususani jitihada za Nairobi na jumuiya ya EAC za kutaka kuleta amani mashariki mwa DRC.
DRC inajiandaa kwa uchaguzi mkuu siku ya Jumatano wiki ijayo. Muungano huu mpya umeongeza hali ya wasi wasi nchini DRC ambayo kwa sasa inakabiliana na makumi ya makundi ya waasi mashariki mwa nchi hiyo.
Kiongozi wa ujumbe wa kikosi cha kutunza amani wa Umoja wa mataifa nchini DRC Bintou Keita, kwenye mtandao wake wa X, amesema kuwa ana wasi wasi mkubwa sana kuhusiana na kuundwa kwa kundi jipya la kijeshi nchini DRC.
Soma zaidi: