Matokeo ya mapema yanaonesha kwamba mgombea wa Muungano wa Azimio raila Odinga amekuwa akitatizika kupata asilimia 20 ya kura zilizopigwa katika maeneo mengi ya mlima Kenya ikiwemo Murang’a, Kiambu, Meru, Kirinyaga na kaunti nyingine zilizo na idadi kubwa ya kura katika eneo la Mlima Kenya.
Katika Kura iliyorekodi idadi ndogo ya wapiga kura, suala muhimu la ni nani ambaye atapata uungwaji mkono katika ngome ya mwingine ndio litaamua ni nani ataibuka mshindi.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Wafula Chebukati, hakutoa matokeo kuhusu kura ya Urais katika kituo kikuu matokeo ya Uchaguzi cha Bomas.
Hata hivyo matokeo ya mapema ya kura za urais zilizotoka kutoka maeneo tofauti nchini yalionesha Bwana William Ruto akiwa anachuana na mpinzani wake mkuu Raila Odinga.
Huku wagombea wengine wawili George Wajackoyah na David Waihiga wakijipatia asilimia 0.5 ya jumla ya kura hizo kati yao, Wagombea wawili wakuu wamekuwa wakibadilishana uongozi kufikia asilimia 50 ya kura zilizohesabiwa.
Kama ilivyotarajiwa Bwana Ruto alitawala katika majimbo ya Bonde la Ufa na Mlima Kenya, huku naye Odinga akipata uungwaji mkono kutoka Nyanza pamoja na Eneo la Mashariki na Pwani.