Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uchaguzi DRC: Mchuano ni mkali kati ya Tshisekedi na Katumbi

Katumbizzz (1).jpeg Uchaguzi DRC: Mchuano ni mkali kati ya Tshisekedi na Katumbi

Wed, 20 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Watu milioni 40 waliojiandikisha kupiga kura, Uchaguzi Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), asilimia 55, wanatarajiwa kumrejesha Felix Tshisekedi kwenye kiti cha urais kwa muhula wa pili. Uchaguzi unafanyika leo, Desemba 20, 2023.

Ripoti yenye kurasa 11, iliyoandaliwa na Taasisi ya Utafiti ya GeoPoll, imeonyesha kuwa wananchi wengi DRC hawana furaha kwa jinsi hali ya mambo ilivyo. Pamoja na hivyo, wengi hawaamini matokeo tofauti endapo Ikulu ya DRC, Palace of the Nation, itakaliwa na mtu mwingine.

Kwa mujibu wa GeoPoll, mambo sugu ambayo wananchi wa DRC wanaona hayaendi sawa ni ajira, usalama, gharama ya maisha, miundombinu (hasa barabara), huduma za afya, rushwa na kadhalika. Matarajio yao ni mshindi wa kiti cha urais abadilishe hayo na kushusha bei za vyakula.

Mkuu wa Kitivo cha Siasa, Chuo Kikuu Katoliki, DRC, Profesa Albert Malukisa, alipofanya mazungumzo hivi karibuni na Al-Jazeera, alisema kuwa mlango wa Tshisekedi kuingia muhula wa pili ni mgumu kwa sababu anakabiliana na mwanasiasa mwenye nguvu, Moise Katumbi.

Profesa Malukisa alifafanua kuwa umaarufu wa Tshisekedi umekuwa ukiporomoka kadiri tarehe ya uchaguzi inavyobisha hodi. Akaongeza: “Mmoja kati ya hao wawili (Tshisekedi na Katumbi), anaweza kushinda kiti cha urais.

Wafuasi wake humwita “Fatshi”, kifupi cha Felix Antoine Tshisekedi Tshilombo. Mwaka 2018 alipokuwa anagombea urais, hakuwa tishio, zaidi alionekana kubebwa na nyota ya baba yake, marehemu Etienne Tshisekedi ambaye Wacongo wa Kinshasa humwita ‘Baba wa Demokrasia’.

Tshisekedi baba, ni alama ya mapambano ya kidemokrasia DRC kwa zaidi ya miongo mitano. Alisimama jicho kwa jicho na dikteta Mobutu Sese Seko. Alikabiliana ana kwa ana na Laurent Kabila. Alipambana hoja kwa hoja na Joseph Kabila – mtoto wa Laurent. Tshisekedi baba, alifariki dunia Februari Mosi, 2017, kwa maradhi ya mapafu.

Fatshi, akionekana kuwa mgombea chaguo la tatu, baada ya Emmanuel Shadary wa kilichokuwa chama tawala, PPRD na Martin Fayulu, aliyepeperusha bendera ya muungano wa Lamuka, matokeo yalipotangazwa, yalimshangaza kila mtu. Fatshi “Tshisekedi” wa UDPS, alishinda urais.

Nadharia kuwa Fatshi aliingia makubaliano ya siri na rais aliyekuwa madarakani, Joseph Kabila, Kanisa Katoliki kumtangaza Fayulu kuwa mshindi halali, ongezea na Fayulu mwenyewe kugoma kuyatambua matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi (Ceni), hakuna kilichobadilika, Fatshi alikula kiapo kuiongoza DRC.

Sasa tena, Fatshi yupo kwenye mapambano ili kurejea madarakani muhula wa pili. Usalama wa nchi ni agenda muhimu, kutokana na eneo la Mashariki ya nchi hiyo, kukumbwa na ghasia nyingi. Vikundi vingi vyenye silaha vimeweka maskani eneo hilo.

Wagombea wawili wa urais, Patrice Majondo Mwamba na Joelle Bile, wameshajiondoa kwenye kinyang’anyiro na kumuunga mkono Fatshi. Hatua hiyo imetafsiriwa kama nyongeza ndogo ya mtaji wa kisiasa kwa Fatshi, kipindi cha lala salama.

Mafanikio ya sekta ya elimu ni turufu inayombeba Fatshi. Kwa msaada wa dola 800 milioni (Sh2.1 trilioni) kutoka Benki ya Dunia, DRC imeandikisha watoto milioni 4.5 kuanza shule ya msingi na kuajiri walimu 36,000.

Hiyo ni hatua ya kihistoria DRC.

Katumbi, baada ya vikwazo vya hapa na pale, vilivyomzuia kugombea urais nyakati zilizopita, kutoka kifungo jela, vitisho vya kuuawa hadi kuishi uhamishoni nje ya nchi, hivi sasa ukungu umetoweka.

Jina na sura yake ni maudhui kwenye karatasi ya kupigia kura, kinyang’anyiro cha urais. Bilionea wa madini, Gavana wa zamani wa jimbo la Katanga na mmiliki wa Klabu ya Soka ya TP Mazembe.

Uchaguzi Mkuu 2018, Katumbi alikuwa akiishi uhamishoni na alimuunga mkono Fayulu. Safari hii, Katumbi anasimama kwa kujiamini, anahitaji kumpumzisha Fatshi na kuchukua kijiti cha uongozi.

Wagombea wanne wa urais wameshajiengua na kutangaza kuelekeza karata zao kwa Katumbi. Franck Diongo, Seth Kikuni, Delly Sesanga na Matata Mapon, ambaye alikuwa Waziri Mkuu mwaka 2012 hadi 2016, ni wagombea waliojisalimisha kwa Katumbi.

Baada ya wagombea sita kujitoa na kujisalimisha kwa Fatshi na Katumbi, mchuano umebaki wa watu 20. Ukiacha majina hayo mawili yenye kupewa nafasi kubwa ya ushindi, wengine ni Fayulu, Tony Bolamba, Jean-Claude Baende na Marie-Josée Ifoku.

Wamo pia mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel 2018, Denis Mukwege, Adolphe Muzito (Waziri Mkuu kati ya 2008–2012), Enoch Ngila, Theodore Ngoy, Radjabho Soborabo, Noel Tshiani, Constant Mutamba, Justin Mudekereza, Georges Falay, Rex Kazadi, Abraham Ngalasi, Nkema Bokonzi, Floribert Anzuluni na Andre Masalu.

Jicho la ulimwengu

DRC inamiliki asilimia 70 ya hifadhi yote ya madini ya coltan, ambayo yanatumika kutengenezea simu. Asilimia 30 ya almasi yote ulimwenguni inatoka DRC. Ongezea utajiri mwingine mkubwa wa shaba, cobalt na bauxite.

Hazina hiyo asilia iliyopo DRC, ni kichocheo cha jicho la ulimwengu kuelekea nchini humo, kufuatilia hali na hatima ya kisiasa. Bila mazingira bora ya kiutawala na usalama, mnyororo wa dunia kunufaika kupitia maliasili kutoka nchi hiyo, hautanyooka ipasavyo.

Utajiri huo wa madini kwa sehemu kubwa upo Mashariki ya DRC, eneo ambalo limekuwa na machafuko kwa zaidi ya miongo mitatu. Mwaka 2008, Kamati ya Kimataifa ya Uokoaji (IRC), ilitoa ripoti kuwa watu milioni 5.4 walipoteza maisha ndani ya miongo miwili, kutokana machafuko Mashariki ya DRC.

Wachambuzi wa masuala ya kibinadamu, walitafsiri ripoti hiyo kuwa vifo hivyo Mashariki ya DRC ni vingi zaidi, tangu ulimwengu ulipotoka kwenye Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Sababu ya vifo hivyo ni matokeo ya mapigano ya silaha, njaa na magonjwa.

Ni miaka miwili sasa tangu Serikali ilipotangaza udhibiti wa kuingia na kutoka kwenye majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri, lakini mapigano hayajakoma. Hali ya usalama ni mbaya. Vikundi vya uasi, M23, Allied Democratic Forces (ADF) na Codeco, vinaendelea kushambulia raia wa kawaida na askari.

Ghasia hizo zimeifanya DRC kuweka rekodi ya idadi kubwa zaidi ya watu kulazimika kukimbia makazi yao. Inakadiriwa watu milioni 6.9, wamehama makazi yao tangu Machi 2022.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa inaeleza kuwa asilimia 39 ya watu hao wamekimbia Ituri na asilimia 28, wameondoka Kivu Kaskazini.

ADF ni wapiganaji ambao ngome yao ni mpaka wa DRC na Uganda, wana nasaba pia na wanamgambo wa Dola ya Kiislamu Iraq na Syria (ISIS). M23, ni waasi mpakani mwa DRC na Rwanda. Nadharia ya muda mrefu ni kuwa Rais wa Rwanda, Paul Kagame, ndiye jeuri kuu ya M23.

Bila shaka, nadharia hiyo kuwa Kagame ndiye godfather wa M23, ni sababu hivi karibuni, Fatshi akiwa Goma, mji mkuu wa Kivu Kaskazini, katika mkutano wa kampeni, alimfananisha Rais huyo wa Rwanda na mtawala wa zamani wa Ujerumani, Adolf Hitler.

Fatshi alimtabiria Kagame anguko kama la Hitler.

Kauli hiyo imetajwa kumwongezea Fatshi umaarufu wa kisiasa. Hivi sasa wafuasi wake wanamwita “Kiboko ya Kagame”. Pamoja na hivyo, wananchi Mashariki ya DRC, wanalaumu hali ya usalama imekuwa mbaya mno kipindi cha Fatshi, afadhali wakati wa uongozi wa Joseph Kabila.

Katumbi, akiongoza muungano wa “Pamoja kwa ajili ya Jamhuri”, amepita katikati ya hali hiyo tete kiusalama.

Ahadi yake kubwa ni kwamba suluhu ya kudumu ya matatizo ya kiusalama Mashariki ya DRC ni yeye kushinda kiti cha urais. Ameahidi kumaliza migogoro yote.

Demokrasia inatambaa

Tangu Februari 18, 2006, Katiba ya DRC ilipopita kwa matumizi, nchi hiyo itafanya uchaguzi wa nne. Wa kwanza ulikuwa Julai 30, 2006. Ukafuata wa Novemba 28, 2011, kisha Desemba 30, 2018. Ni mara ya kwanza DRC wanafanya uchaguzi tangu nchi hiyo ilipofanya mabadilishano ya kwanza ya utawala kwa amani. Kutoka Joseph hadi Fatshi.

Kabla ya Uchaguzi Mkuu 2006, DRC ilikuwa imepitisha miaka 22 bila kufanya uchaguzi.

Mara ya mwisho wananchi kusimama vituoni kupiga kura ilikuwa Julai 28, 1984, kipindi hicho mgombea urais alikuwa mmoja tu, Mobutu.

Baada ya uhuru wa DRC, Juni 30, 1960, nchi hiyo ilifanya uchaguzi wa vyama vingi Machi na Aprili 1965, kisha Mobutu akaiteka nchi kijeshi.

Akafuta vyama vyote vya siasa. Novemba Mosi, 1970, wananchi walipiga kura za “ndiyo” na “hapana” kwa mgombea pekee aliyekuwepo, ambaye ni Mobutu.

Utaratibu huo ukafanyika mwaka 1977 na 1984. Kimahesabu, tangu uhuru, leo DRC wanafanya uchaguzi kwa mara ya nane. Wapinzani wanaingia kwenye uchaguzi wakiwa hawana imani na Ceni (Tume).

Delly Sesanga ambaye ni mgombea urais aliyejitoa na kumuunga mkono Katumbi, alitoa tamko mapema kuwa matokea yatakayotolewa na Kanisa Katoliki ndiyo atayaamini kuliko ya Ceni. Fatshi, analaumiwa kwa kujaza watu wake ndani ya Ceni, akiwemo Rais wa Tume hiyo, Dk Kadima Kazadi.

Vilevile Fatshi anakosolewa kwa kuteua majaji wa Mahakama nchini humo bila kufuata utaratibu.

Mshindi wa kiti cha urais ataapishwa Januari 20, 2023 jijini Kinshasa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live