Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uchaguzi DRC 2023: Rais Felix Tshisekedi atangazwa kushinda kwa kishindo

Uchaguzi DRC 2023: Rais Felix Tshisekedi Atangazwa Kushinda Kwa Kishindo Uchaguzi DRC 2023: Rais Felix Tshisekedi atangazwa kushinda kwa kishindo

Mon, 1 Jan 2024 Chanzo: Bbc

Rais Félix Tshisekedi ametangazwa mshindi wa uchaguzi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambao umelaaniwa kuwa ni "uzushi" na wagombea kadhaa wa upinzani wanaodai yafanyike marudio ya uchaguzi huo.

Rais alishinda takribani 73% ya kura, huku mpinzani wake wa karibu, Moise Katumbi, akipata 18%, maafisa walisema.

Uchaguzi wa Desemba 20 ulikumbwa na matatizo mengi ya vifaa.

Ilibidi iongezwe hadi siku ya pili katika baadhi ya maeneo.

Takribani theluthi mbili ya vituo vya kupigia kura vilichelewa kufunguliwa, wakati asilimia 30 ya mashine za kupigia kura hazikufanya kazi siku ya kwanza ya upigaji kura, kwa mujibu wa waangalizi wa uchaguzi.

Mamilioni ya watu walisubiri kwa saa nyingi kabla ya kupiga kura, huku wengine wakikata tamaa na kurudi nyumbani.

Upinzani ulisema matatizo hayo ni sehemu ya mpango wa makusudi wa kuruhusu matokeo kuchakachuliwa ili kumpendelea Bw Tshisekedi, mwenye umri wa miaka 60.

Wapinzani kadhaa wakuu wameitisha maandamano baada ya matokeo kutangazwa.

"Tunatoa wito kwa watu wetu kujitokeza barabarani kwa wingi baada ya kutangazwa kwa udanganyifu katika uchaguzi," walisema katika taarifa ya pamoja Jumapili.

Jeshi limetumwa katika maeneo mbalimbali ya mji mkuu Kinshasa ili kuzuia ghasia zozote.

Mkuu wa tume ya uchaguzi hapo awali alisema wagombea wa upinzani wanataka uchaguzi mpya kwa sababu "wanajua walishindwa ... ni walishindwa vibaya".

Mkuu wa Tume ya Uchaguzi Denis Kadima alikiri kuwepo kwa dosari kadhaa lakini akasisitiza kuwa matokeo yanaakisi matakwa ya watu wa Congo.

Tajiri wa kandanda na gwiji wa katika sekta ya madini Bw Katumbi aliibuka wa pili kwa 18% ya kura, huku Martin Fayulu, ambaye alidai kuporwa ushindi katika uchaguzi wa mwaka 2018, alikuwa wa tatu kwa takribani 5%.

Hakuna hata mmoja wa wagombea wengine 17 aliyepata zaidi ya 1% ya kura. Bw.Kadima alisema waliojitokeza kupiga kura ni takribani 43% ya wapiga kura milioni 41 waliojiandikisha.

Haijabainika kama kuna mgombea kati ya 18 wa upinzani atapinga matokeo hayo mahakamani. Bw Katumbi tayari amesema haina maana kwa sababu mahakama haziko huru.

Mahakama ya Katiba ina siku 10 za kusikiliza pingamizi lolote la kisheria kabla ya kutangazwa kwa matokeo ya mwisho tarehe 10 Januari 2024.

DR Congo ni takribani mara nne ya ukubwa wa Ufaransa, lakini haina miundombinu muhimu. Hata baadhi ya miji yake mikuu haijaunganishwa na barabara.

Takriban theluthi mbili ya wakazi milioni 100 nchini humo wanaishi chini ya mstari wa umaskini, wakipata $2.15 (£1.70) kwa siku au chini ya hapo.

Wapiga kura pia walichagua wawakilishi wa ubunge, mkoa na manispaa, wakiwa na wagombea wapatao 100,000 kwa jumla.

Uchaguzi huo haukufanyika katika baadhi ya maeneo ya mashariki kwa sababu ya mapigano ambayo yamekuwa yakiendelea katika eneo hilo kwa miongo mitatu iliyopita.

Makumi ya makundi yenye silaha yamekuwa yakipambana kudhibiti maeneo yenye utajiri mkubwa wa madini nchini humo.

Chanzo: Bbc