Marekani imetoa tahadhari ya usalama kwa raia wake nchini Kenya kuhusu mashambulizi ya kigaidi yanayoweza kutokea nchini humo.
Ujumbe huo unaonya kuwa hoteli, balozi, mikahawa na maduka makubwa yanayotembelewa na wageni na watalii yanaweza kushambuliwa.
Haya yanajiri saa chache baada ya mamlaka nchini Kenya kutangaza majina ya wanaume watano wanaosakwa kwa ajili ya kuwa na uhusiano na kundi la Al Shabab.
Watano hao wameorodheshwa miongoni mwa watu wanaosakwa zaidi nchini Kenya kwa madai ya mashambulizi yaliyotekelezwa katika mji wa pwani wa Lamu.
Kundi hilo la kijihadi limelaumiwa kwa kufanya mashambulizi Kaskazini na pwani ya Kenya likilenga raia, maafisa wa usalama na vituo vya serikali.
Kundi tanzu la Al Qaeda limepata hasara kubwa katika siku za hivi karibuni, likiwapoteza makamanda wakuu, mamia ya wapiganaji na maeneo makubwa ya maeneo ya kati na Kusini mwa Somalia ambako wamekuwa wakidhibiti kwa miongo kadhaa.