Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uamuzi wa mwisho FDI bomba la mafuta mwakani

Dbc71d2fd257cf610f7258ebcf625169 Uamuzi wa mwisho FDI bomba la mafuta mwakani

Tue, 24 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAZIRI wa Maendeleo ya Nishati na Madini Uganda, Mary Kitutu ametangaza rasmi kuwa uamuzi wa mwisho kuhusu uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje (FID) katika mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) utafanyika katika robo ya kwanza ya mwaka ujao.

Hatua hiyo ni ya mwisho kabla ya kuanza rasmi ujenzi wa bomba hilo lenye urefu wa kilomita 1,445 ambalo litasafirisha mafuta ghafi kutoka Kabaale nchini Uganda hadi Rasi ya Chongoleani iliyo karibu na Bandari ya Tanga nchini Tanzania.

Akizungumza katika mkutano wa sekta ya mafuta na gesi wa Afrika Mashariki wa mwaka huu uliofanyika kwa njia ya mtandao kutokana na janga la corona, Kitutu alisema mwaka huu umekuwa na changamoto nyingi katika mradi huo kutokana na janga la corona ambalo limeathiri vibaya sekta ya mafuta na gesi.

“Kwa kuwa shughuli zimeanza kwenda vizuri nina matumaini kwamba kufikia robo ya kwanza ya 2021, FID itakuwa imefanywa, tunafanya kazi kwa bidii kuifanikisha. Bomba hilo la kihistoria Afrika Mashariki ni la uwekezaji wa zaidi ya dola za Marekani bilioni 3.5.”

“Mradi huu utatoa fursa nyingi za kibiashara ndani ya nchi na ukanda mzima wa Afrika Mashariki na ndio mkataba mkubwa zaidi wa kibiashara kati ya Uganda na Tanzania,” alisema.

Akizungumzia fursa zilizopo kwenye mradi huo, Kitutu alisema serikali ya Uganda inatoa nafasi kwa kampuni za ndani kushiriki katika mradi huo na inafanya kazi kwa karibu na Chama cha Wachimbaji Madini Uganda na vyama vingine vya sekta hiyo ili kuhakikisha kampuni za nchi hiyo zinashiriki.

Alisema serikali imetenga nyongeza ya ziada ya dola za Marekani bilioni 20, kiasi ambacho kitatumika kusaidia kampuni za nchi hiyo katika maeneo ya miradi ya mafuta na gesi.

Serikali za Uganda na Tanzania zilisaini makubaliano ya mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) Mei 2017 na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa bomba hilo Agosti mwaka huo huo.

Mradi huo hata hivyo haukuweza kuendelea kutokana na masuala ya kisheria na mazingira.

Septemba mwaka huu Uganda na Tanzania zilisaini Mkataba wa Serikali Wenyeji (HGA) ili kuharakisha maendeleo ya mradi huo.

Ujenzi wa mradi huo unatekelezwa kwa ubia kati ya kampuni ya Total (asilimia 66.7) na CNOOC (asilimia 33.3).

Bomba hilo la kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki litakuwa na uwezo wa kusafirisha mapipa 216,000 ya mafuta ghafi kwa siku.

Chanzo: habarileo.co.tz