Takriban Wanigeria milioni 25 wako katika hatari ya kukabiliwa na njaa kati ya mwezi Juni na Agosti mwaka huu ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa.
Hayo ni kwa mujibu wa tathimini ya chakula na lishe iliyofanywa Oktoba 2022 na asasi ya Cadre Harmonisé inayoongozwa na serikali na kuungwa mkono na Umoja wa Mataifa.
Tathmini hiyo inayofanyika mara mbili kwa mwaka ikisaidiwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF inasema, hilo ni ongezeko linalokadiriwa kwa wastani wa watu milioni 17 walio katika hatari ya uhaba wa chakula kwa sasa.
Tathimini hiyo imesema “kuendelea kwa migogoro, mabadiliko ya tabianchi, mfumuko wa bei na kupanda kwa bei za vyakula ni vichochezi muhimu vya mwelekeo huu wa kutisha.”
Kwa mujibu wa tathmini hiyo, upatikanaji wa chakula umeathiriwa na ghasia zinazoendelea katika majimbo ya kaskazini-mashariki ya Borno, Adamawa na Yobe (BAY) na ujambazi wa kutumia silaha na utekaji nyara katika majimbo kama vile Katsina, Sokoto, Kaduna, Benue na Niger.
Kulingana na shirika la kitaifa la kusimamia masuala ya dharura, mafuriko yaliyoshamiri katika msimu wa mvua wa mwaka 2022 yaliharibu zaidi ya ekari 676,000 za mashamba, ambayo yalipunguza mavuno na kuongeza hatari ya uhaba wa chakula kwa familia kote nchini Nigeria.
Kwa mujibu UNICEF watoto ndio walio hatarini zaidi kutokana na uhaba wa chakula.
Takriban Wanigeria milioni 6 kati ya milioni 17 wasio na chakula leo hii ni watoto wa chini ya umri wa miaka 5 wanaoishi katika majimbo ya Borno, Adamawa, Yobe, Sokoto, Katsina na Zamfara