Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR, limesema limesikitishwa sana na mapigano makali kati ya makundi yasiyo ya kiserikali yenye silaha na vikosi vya serikali yanayowafanya mamia kwa maelfu ya watu kuyakimbia makazi yao Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Ijumaa na msemaji wa shirika hilo Matthew Saltmarsh mjini Geniva Uswisi wakati wa mkutano na waandishi wa habari “Mwezi Februari pekee, karibu watu 300,000 walikimbia katika maeneo ya Rutshuru na Masisi katika jimbo la Kivu Kaskazini.”
Ghasia zimeongezeka hususan kuanzia mkoa wa Kitchanga katika eneo la Masisi kuelekea mji muhimu kimkakati wa Sake, huku watu 49,000 wakilazimika kuyahama makazi yao katika wiki ya tarehe 17 Februari.
Katika wilaya ya Kibirizi katika eneo la Rutshuru, watu wengine 20,000 walikimbia wiki ya tarehe 6 Machi.
UNHCR inasema raia wanaendelea kupata hasara kubwa kutokana na umwagaji unaonedelea, ikiwa ni pamoja na wanawake na watoto ambao walitoroka kwa shida kwenye ghasia na sasa wanalala hadharani katika maeneo ya wazi huku wakiwa wamechoka na wakiwa na kiwewe.
Zaidi ya watu 5,500 pia wamevuka mpaka na kuingia nchi jirani ya Rwanda tangu Januari, na wengine 5,300 wameingia Uganda huku ukosefu wa usalama na ghasia zikiendelea kukumba mikoa ya mpakani.
UNHCR inasisitiza wito wake kwa wahusika wote wa vita Mashariki mwa DRC kukomesha ghasia ambazo zinaathiri raia kwa kiasi kikubwa.
DRC ndio yenye mzozo mkubwa zaidi wa wakimbizi wa ndani barani Afrika, huku watu milioni 5.8 wakiwa wakimbizi wa ndani, haswa Mashariki mwa nchi hiyo.
Kwa mwaka wa 2023, UNHCR inaomba dola milioni 232.6 kusaidia wakimbizi wa ndani na wakimbizi wengine walioko nchini DRC. Hadi kufikia sasa operesheni za misaada za UNHCR nchini DRC zimefadhiliwa kwa asilimia 8 pekee.
Wakati huo huo, Ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa umewasili nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Ijumaa, ikiwa ni sehemu ya ziara ya kikazi ya kutathmini hali ya usalama na utekelezaji wa majukumu ya vikosi vya umoja wa mataifa vya kulinda mamani nchini humo MONUSCO.
Wajumbe hao watakutana na watu kutoka tabaka mbali mbali ikiwemo mashirika ya kiraia na Rais wa DRC Félix Tshisekedi jijini Kinshasa na baadae watakwenda mjini Goma jimboni Kivu Kaskazini, ambako mapigano yamezidi kurindima kwa miezi kadhaa sasa kati ya jeshi la serikali na kundi la wanamkambo wa M23.